Mzee Mwinyi: Rais Magufuli Amefanya Mambo Mengi Yaliyokuwa Yameshindikana Kwa Miaka Mingi


Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Mzee Ally Hassan Mwinyi amesema katika kipindi cha uongozi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli, nchi imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuushangaza ulimwengu.

Akitoa salamu jana March 27, 2021 katika uwanja wa Magufuli wilayani Chato mkoani Geita ilipofanyika Misa Takatifu ya Mazishi ya Dkt Magufuli, Mzee Mwinyi alisema kiongozi huyo alikuwa si mtu wa maneno, bali alikuwa  mtu wa vitendo na aliyependa matokeo.

Mzee Mwinyi alisema katika kipindi kifupi cha takribani miaka mitano Dkt Magufuli ameweza kufanya mambo makubwa ambayo watangulizi wake walishindwa kuyafanya kwa takribani miaka 40 , ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo ndoto ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma.

Mambo mengine ni kuiunganisha Tanzania kwa barabara za lami na kuboresha usafiri wa anga kwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Rais Mstaafu Mwinyi alisema kifo cha Dkt Magufuli binafsi kimemsikitisha sana, kwani alikuwa ni kiongozi aliyempenda sana.


from MPEKUZI

Comments