Waziri Ummy achukizwa uchafu wa mazingira kiwanda cha Saruji


 Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amesikitishwa na hali ya uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda cha kuzalisha simenti , jijini Tanga na kushindwa kuvumilia hali hiyo inayowaathiri wananchi waishio jirani.

Hali hiyo inayotokana na vumbi na gesi chafu imekua ikiwatesa wananchi pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Donbosco ambayo iko jirani zaidi na kiwanda hicho ambapo pia athari kubwa imeshaonekana kwa wanafunzi na walimu wao kwani wanaugua mara kwa mara magonjwa yatokanayo na hali hiyo.

Waziri Ummy alisema kuwa pamoja na kuhitaji wawekezaji wa viwanda nchini lakini pia afya njema inahitajika kwa wananchi wake ili kujenga Taifa imara na lenye nguvu, lakini pia alienda mbali zaidi na kufanya tathmini ya haraka na kuona kiwqnda kwa mwezi kinaingiza mapato makubwa lakin pia wananchi wanaathirika, hata hivyo aliagiza taasiai ya NEMC kuchunguza hali hiyo ndani ya wili moja.

"Wawekezaji tunawataka kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa lakini pia wananchi wanahitaji kua na afya njema ili kua na Taifa imara lenye nguvu, naagiza NEMC ndani ya siku saba mje hapa mfanye uchunguzi kujua hii hali ina athari kiasi gani, hatutaki kupoteza mapato ya kiwanda lakini tunahitaji hawa watoto wetu  hapa wawe na afya njema " alisema.

Awali akitoa taarifa ya Meneja wa shule hiyo Sebastiana Mlacha alitoa malalamiko yao na kusema kuwa athari ni nyingi ambazo mbali na kuugua hali hiyo imewasababishia hasara kubwa ya wanafunzi kuhama kila mwaka kutokana na kuugua mara kwa mara.

Mlacha alifafanua kwamba uongozi wa shule ulishatoa taarifa za athari wanazopata kwa viongozi wanaohusika na mazingira lakini wanaishia kutoa ahadi ya kulifanyia kazi bila mafanikio, huku kiwanda kuendelea na uzalishaji kama kawaida.

"Tarehe 9/12/ 2020  kulitokea tena vumbi la ajabu jeusi, tulipiga picha sehemu zote tukamrushia Meneja wa kanda wa NEMC, tuliwasiliana nae na kumweleza hali halisi na jinsi tunavyoteseka, akaahidi kulifanyia kazi haraka, tarehe 7/ 1/ 2021 meneja alitutembelea na timu yake ambapo walijionea hali ilivyokua mbaya, wakaahidi kulifanyia kazi" alisema Mlacha.

Aidha alibainisha kwamba wanafunzi wengi wamehama shuleni hapo ambapo kwa mwaka huu badala ya wanafunzi wapatao 151 kuanza kidato cha kwanza walihama na kubaki wasiozidi 50 na kuongeza kwamba tatizo hilo limekuwa la muda mrefu huku wakiambiwa kiwanda hicho kitafanyiwa marekebisho lakini hakuna mabadiliko.

"Mheshimiwa Waziri utusaidie, ni ukweli mtupu kwamba tunahitaji viwanda ili kuinua uchumi wetu lakini binadamu ana thamani kubwa sana kuliko fedha, tunanyanyasika, tunateseka sana na vumbi, wanafunzi wetu wengi wamehama kwa ajili ya kuumwa macho, kujikuna na kukohoa, tunaonba suala letu ulipatie ufumbuzi" aliongeza.


from MPEKUZI

Comments