Waziri Simbachawene Awasweka Rupango Viongozi Wa Vijiji Kwa Kushawishi Vurugu Wafugaji, Wakulima Kiteto


Na Mwandishi Wetu, MOHA, Kiteto
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameamuru kukamatwa na kuwekwa mahabusu viongozi wa vijiji vya Miriongima na Kijungu Wilayani Kiteto kwa kosa la kushawishi wananchi kufanya vurugu na kuvamia eneo lililotengwa na Serikali kwa shughuli za mifugo.

Viongozi hao ambao pia wapo upande wa wakulima, wanadaiwa kuchukua rushwa kwa kuuza mashamba ambayo yapo maeneo ya wafugaji na kusababisha kuibuka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika vijiji vya Kijungu na Amei.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kitongoji cha Miriongima, Kijiji cha Kijungu, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, leo, Waziri Simbachawene alisema viongozi hao wa vijiji ndio wanaochochea migogoro ambayo inaendelea kwasababu wanawadanganya wananchi na kupelekea kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa shughuli za mifugo kwa kufanya kilimo.

 “Nimekuja kwasababu ya uvunjifu wa amani, nimekutana na viongozi wenu wa Wilaya na Mkoa, pia nimetembelea Kijiji cha Amei, na nyie hapa nimewasikiliza, kwa wale ambao mlienda kulima kule ardhi ya kijiji cha Amei, mkiamini kwamba viongozi hawa wa kijiji cha Kijungu ni wakweli, sasa muelewe kuanzia leo kwamba wamewadanganya ile ardhi sio yao kwasababu shamba hilo la Jumuiya lilishakufa siku nyingi na vijiji vilishaanzishwa, Mwenyekiti wa Kitongoji hiki, na Mwenyekiti wa Kijiji hiki wanatakiwa kuchukuliwa hatua,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa; “….kwasababu kama viongozi hawa wangekuwa na madai ya msingi, Mkuu wa Wilaya ungeyajua, Mkuu wa Mkoa ungeyajua, Mkurugenzi angeyajua, Mwenyekiti wa Halmashauri angeyajua, lakini dai la mkologanyo la mpaka haliwezi likaja leo wakati kumetokea hilo, niwaambieni wale ambao mlidanganywa, mkaawaamini hawa, na mkaenda kufanya kule kilimo, mlifanya kwa hiari yenu, na hasara nmi yenu, poleni, kwenye ukweli lazima tuseme ukweli.”

Waziri huyo alisisitiza kuwa, haiwezekani Mwenyekiti wa Kijiji cha Kijungu kutokujua kuwa kuna Kijiji cha Amei, na kijiji hicho kilianzishwa tangu mwaka 1993, viongozi hao ni wachonganishi, na pia wameshindwa hata kukaa na Mwenyekiti wa Amei kuzungumza suala hilo ambalo lipo kisheria.

Waziri Simbachawene aliambatana na viongozi wa mbalimbali wa Wilaya na Mkoa, ambao ni Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati yake ya Usalama ya Wilaya, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, pamoja na viongozi wa halmshauri ya Wilaya hiyo.

Aidha, Waziri Simbachawene kwa niaba ya Serikali aliagiza uongozi wa Wilaya na Mkoa, kuhakikisha viongozi wa vijiji wanaosababisha migogoro wanakamatwa na kuchukluliwa maelezo kwa kuwa imebainika migogoro mingi ndani ya Wiklaya ya Kiteto, ya kuuza maeneo ambayo tayari yana mipango bora ya matumizi ya ardhi katika Wilaya hiyo, yanasababishwa na viongozi wa Vijiji na Kata.   

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Joseph Mkirikiti, alisema katika kijiji cha Amei, kuna wakulima wakubwa ambao wamewaweka wafanyakazi katika mashamba hayo, na endapo Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wa Wilaya wakienda katika mashamba hayo, wakulima hao wakubwa hawaonekani zaidi ya wanaofanyia kazi.

“Mheshimiwa Waziri kuna watu wakubwa, hawapo zaidi ya watano, mmoja anahekari mia tano, mwingine hekari 2000, mwingine hekari 3000, hawa watu wamelima kule, ukienda kule mashambani hukutani nao, unakutana na watendaji kazi na kuwakamata huwezi, utawaonea, na hatuwezi tatua tatizo, bado tukasisitiza hawa watu waje ofisini ili tuzungumze lakini hawataki kuja,” alisema Mkirikiti.

 Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Ole Lataika, alisema njia pekee ya kuluhisha tatizo hili kati ya Wakulima na Wafugaji ni kusimamia sheria, na ndio njia pekee ya kumaliza suala kwasababu mkulima ni muhimu na mfugaji ni muhimu katika maendeleo.

“Sheria peke yake ndio itatunusuru tukisimamia bila kumuonea mtu yeyote, mkulima ni muhimu na mfugaji ni muhimu, na matumizi bora ya ardhi ndio njia pekee ambayo tumejiwekea, kwamba mkulima atalima hapa na mfugaji atafuga hapa na wale walio na mamlaka wasimamie bila kupindisha hata hatua moja, tukifanya hivyo mambo yote yatakuwa shwari, na mambo yanayoendelea kule yanakuzwa tu, kwa kata mbili, tatu ndio iwe Kiteto nzima sio salama, kuna maeneo mengine wapo wakulima na wagugaji usikii haya mambo hata kidogo,” alisema Lataika.


from MPEKUZI

Comments