Watu wenye silaha waua raia 10 mashariki mwa DRC


Watu wenye silaha wanaodhaniwa ni waasi wa ADF wameuwa watu 10 katika mashambulizi ya nyakati za usiku ya siku mbili tofauti huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jeshi la nchi hiyo limetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, waasi wa ADF waliwakata vichwa wanavijiji wanane wa kijiji cha Boyo cha mkoa wa Ituri huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wakawauwa kwa kuwapiga risasi raia wawili huko Kainama.

Akitoa taarifa hiyo, msemaji wa jeshi la Congo, Luteni Jules Ngongo amesema leo Jumamosi kwamba wanajeshi wa serikali wanaendelea na operesheni za kupambana na waasi hao.

Wakazi wa maeneo hayo wamethibitisha kutokea mashambulizi hayo mawili ya nyakati za usiku na kuongeza kuwa, waasi hao wamechoma pia nyumba za wakazi wa sehemu hizo.

Kainama ni eneo lililoko juu kabisa ya jimbo la Kivu Kaskazini na linapakana na jimbo la Ituri. Liko umbali wa kilomita 5 tu kutoka kijiji cha Boyo. Mikoa yote hiyo miwili ya mashariki mwa Congo, inapakana na Uganda.

Waasi wa ADF ni wa Uganda ambao wameweka kambi zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu mwaka 1995.


from MPEKUZI

Comments