Na. Abdulrahman Salim – Rukwa
Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC) wameiomba Serikali kukamilisha taratibu za kuendeleza ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA Mjini Sumbawanga ili wanafunzi na makundi mbalimbali ya vijana wanaohitaji kuendelea na ufundi katika Chuo hicho kuweza kunufaika nacho na hatimae kuchochea maendeleo ya Mkoa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kukitembelea na kukikagua chuo hicho kabla ya kuanza kikao cha kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa kamati ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wamesema kuwa serikali imeshawekeza fedha za kutosha hadi kufikia hatua hiyo baada ya kuachana na mkandarasi aliyeshindwa kumaliza ujenzi huo na hatimae kukiendeleza kwa utaratibu wa “Force Account”.
Mh. Aida Khenan ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini ambaye kwa upande wake alisema kuwa vijana wengi wanaofaidika na asilimia 10 ya mikopo inayotolewa na halmashauri wanashindwa kuendeleza miradi yao kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kufanya hivyo jambo ambalo lingepunguzwa na uwepo wa chuo hicho mkoani humo.
“Leo tungetemea kwamba ile asilimia 10 inayotolewa na serikali kwaajili ya kukopesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kumekuwa na changamoto ya marejesho ya ile fedha na sababu ni moja tu, wanapewa fedha na hawana mafunzo ya kitu wanachokwenda kufanya ili waweze kurejesha lakini wale wanaotoka hapa ambao wanakuwa tayari wamepewa amafunzo ya namna ya kujitegemea ingekuwa ni rahisi kuwapa wao waweze kujiajiri na kuwaajiri wenzao,” Alisema.
Nae Mbunge wa Kalambo Mh. Josephat Kandege aliiomba serikali kufanya kila kinachowezekana ili chuo hicho kikamilike na pia kutoa kozi ambazo zingewasaidia wananchi wa mkoa wa Rukwa na maeneo jirani.
“Ukiwa unaanzisha chuo cha VETA ambacho hakijatilia maanani kwamba sisi ni wakulima, matrekta yatakuwepo, tunahitaji vijana ambao watakuwa wamefundishwa waweze kuyatengeneza matrekta badala ya kwenda kufuata mafundi mbali itakuwa tunajidanganya na bahati nzuri wamesema kuwa hiyo wataweka katika kozi ambazo zinatakiwa kuwepo,” Alisema.
Aidha, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justin Malisawa aliutaka uongozi wa VETA kuhakikisha mazingira ya eneo hilo yanatunzwa baada ya shughuli za ujenzi kusimama tangu tarehe 14.1.2020 huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone akishauri kamati hiyo kuendelea kufuatilia maendeleo ya chuo hicho ili wananchi wapate walichotaraji.
Wakati akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi huo msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Chuo hicho ch a VETA Jerome Longido alisema kuwa ujezi huo ulitakiwa kumalizika tarehe 22.9.2019 lakini serikali ilimuongezea muda siku 100 mkandarasi Tender International lakini hadi kufikia mwisho wa muda wa nyonyeza tarehe 31.12.2019 mkandarasi huyo alishindwa kukamilisha mradi na hatimae tarehe 14.1.2020 aliandika barua ya kusitisha kuendelea na ujenzi huo ambao mpaka tarehe 23.2.2021 hakuna ujenzi unaoendelea katika eneo hilo.
“Hivi majuzi watu wa Wizara ya Elimu walikuja hapa wakaonesha nia ya kwamba huu mradi ufanyike kwa njia ya ‘force account’ na kuachana na mambo ya mkandarasi, walitoa hayo maelekezo baadaye tukaja na timu ya mkandarasi na mshauri elekezi na sisi VETA tukashirikiana kuona hatua iliyofikiwa ya huu mradi ili kuachana rasmi na mkandarasi, zoezi lilifanyika na makubaliano yamefikiwa, mkandarasi amekubali na sasa kazi imerudi serikalini na sasa mradi utaendeshwa kwa ‘force account’ lakini ni lini utaanza, viongozi wa juu wanajua,” Alisema.
Wakati Mkandarasi anakabidhiwa mradi huo ulikuwa na Gharama za Shilingi Bilioni 10.7 na ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment