Sekta Ya Hifadhi Ya Jamii Kuchochea Kasi Ya Maendeleo Ya Kiuchumi Nchini


 Na. Mwandishi Wetu – Morogoro

Imeelezwa kuwa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikitumika vizuri itawezesha kukuza kasi maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla endapo itawekeza kwenye maeneo au miradi ya kimkakati.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akitoa majumuisho ya ziara yake alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Machinjio ya Kisasa cha Nguru Hills kilichopo Mvomero, Mkoani Morogoro.

Akikagua Mradi huo Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inaitazama sekta ya hifadhi ya jamii kuwa ni chachu ya kukuza kasi ya maendeleo ya uchumi ya Taifa kutokana na uwekezaji mzuri unaofanywa na sekta hiyo katika kuwekeza kwenye maeneo ya kimkakati na miradi mikubwa ya kimkakati inayoanzishwa hapa nchini.

“Tumeshuhudia tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani chini ya Kiongozi wetu mahiri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo kuwa sekta ya hifadhi ya jamii iwe sehemu ya kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza kwenye maeneo ya kimakati ambayo yanatija ama miradi ya kimakati inayoweza kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi,” alieleza Waziri Mhagama

“Ujenzi wa kiwanda hiki cha Machinjio ya Kisasa cha Nguru Hills inaashiria kuwa sasa sekta ya hifadhi ya jamii imeamua kuitikia wito wa ukuzaji wa uchumi wa Taifa kwa kuwekeza kwenye mradi huo ambao utakuwa na tija kubwa,” alisema

Aliongeza kuwa, kukamilika kwa kiwanda hiko kutawezesha uzalishaji wa nyama yenye ubora na ngozi itakayotoka kiwandani hapo kuwa na ubora wa kuuzwa kwenye masoko ya ndani au nje ya nchi na hivyo kuingiza fedha za kigeni ambazo zitawezesha uchumi wa Taifa kukua kwa kasi.

“Kiwanda hiki cha Nguru Hills ni eneo moja wapo muhimu ambalo litatumika kama eneo la kimkakati la kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na mifugo,” alisema Mhagama

Alifafanua kuwa, Serikali imedhamiria katika kipindi hiki cha pili 2020 – 2025 kuongeza viwanda vikubwa vya machinjio ya kisasa ambayo yatakuwa na uwezo wa kuongeza idadi ya ngombe na mbuzi ambao watakuwa wanachinjwa kwa wingi hapa nchini.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alizindua kiwanda cha Ngozi cha Taifa cha Ace Leather Industries kilichopo Mahonda na pia Kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd ambacho ni kiwanda fungamanishi cha bidhaa za ngozi, uwepo wa viwanda hivyo unaanza kufungua fursa kwa wafugaji hapa nchini,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alisema kuwa Kiwanda kitatoa fursa ya ajira za zisizopungua 350 na pia kuwezesha wakazi waliokatika maeneo ya karibu na kiwanda hicho kupata mbolea ambayo itatoa fursa kwa vijana kuanzisha shughuli za kilimo ikiwemo cha mbogamboga ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mhagama aliwataka waratibu wanaosimamia mradi huo kuhakikisha ifikapo Aprili, 2021 mradi huo unakamilika na kukabidhiwa kulingana na makubalianao ya ujenzi huo.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya alieleza kuwa wilaya ya Mvomero ina mifungo mingi hivyo uwepo wa kiwanda hicho kitatoa fursa kwa wafungaji waliopo kwenye maeneo hayo pamoja na kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.

“Wafugaji hapo awali walikuwa wakiuza mifugo yao kwenye minada ya kawaida lakini sasa wataweza kuuza mifugo yao kwenye kiwanda hiki kwa kuwa na soko la uhakika, pia wakazi wa maeneo haya wataweza kupata ujuzi wa masuala mbalimbali katika kiwanda hicho,” alieleza Mgonya

Naye, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Ndg. Fortunatus Magambo alihahidi kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati pamoja na ufungaji wa mashine kwa ajili ya kuanza shughuli za uzalishaji.

Pia alieleza kuwa Kiwanda kina lenga kuwa na uzalishaji mkubwa utakao changia katika uchumi wa nchi na kupata faida ili fedha zilizowekezwa na wanachama kuongezeka thamani.




from MPEKUZI

Comments