Rais Magufuli Ataja Sababu za Kuendelea Kumteua Balozi Kijazi

 Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema alikosa mtu wa kumteua kuwa katibu mkuu kiongozi baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Balozi John Kijazi kustaafu mwaka 2017 na hivyo kuamua kumuongezea muda.

Magufuli amefichua siri hiyo leo Ijumaa Februari 19, 2021 katika ibada ya mazishi ya Balozi Kijazi aliyefariki dunia juzi usiku Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu.

Magufuli amesema Balozi Kijazi aliyezaliwa mwaka 1956 umri wake wa kustaafu ulifika mwaka 2017 na alilazimika kuendelea kufanya naye kazi kutokana na kukosa mbadala wake.

“Alizaliwa mwaka 1956 lakini mpaka leo alikuwa bado ni katibu mkuu kiongozi, maana yake ulipofika wakati wa kustaafu mwaka 2017 nikajaribu kuangalia nani wa kuchukua nafasi yake nikakosa.”

“Nikamuongeza miaka miwili nikifikiri ndani ya muda huo nitapata mwingine lakini hadi mwaka 2019 sikupata, nikamuongeza tena miaka mingine miwili, Mungu akasema umezoea kweli akamtumie yeye mwenye,” amesema Rais  Magufuli

Alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa familia, mke wa marehemu na  watoto huku akibainisha kuwa Kijazi alikuwa mtu mwenye upendo mkubwa na alimpenda Mungu na siku za Jumapili hakukosa kanisani.



from MPEKUZI

Comments