RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba ile ndoto yake ya kuifanya Zanzibar iwe ni sehemu ya kutoa tiba za kibingwa sasa imeanza.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo jana wakati alipowapongeza madaktari wa Kitengo cha upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu cha Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar ambao aliwaaita Ikulu Jijini Zanzibar kwa lengo hilo maalum la kuwapongeza.
Pongezi hizo zimekuja mara baada ya kitengo hicho cha wataalamu hao kumfanyia upasuaji mgonjwa Kelesh Belinda raia kutoka nchini Nigeria ambaye hakuwa na imani ya kutibiwa hapa Zanzibar lakini kutokana na uwezo uliopo wa kitengo hicho cha hapa Zanzibar mgonjwa huyo aliweza kutibiwa na hatimae mara baada ya kupona alianza kuipa sifa Zanzibar na kutoa taarifa katika mitandao ya kijamii.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna haja ya kuwapongeza madaktari hao kwa kuanza kutoa huduma hizo za kibingwa ambazo ni ngumu jambo ambalo wameonesha kwamba inawezekana katika kutekeleza ndoto zake.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alikipongeza kitengo hicho cha Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kazi nzuri wanazozifanya ambazo zimepelekea kuwaita Ikulu kutokana na mafanikio waliyoyapata ambayo yameijengea sifa kubwa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna haja ya kuwapongeza kutokana na kazi hizo licha ya kutambua kwamba wanafanya kazi hizo katika mazingira magumu kwani nia ya kurekebisha mazingira magumu ipo.
Alisema kwamba kazi inayofanywa na kitengo hicho ni kutoa tiba kwani wagonjwa wengi waliokuwa wakisafirishwa kwenda Dar-es-Salaam ama nje ya nchi hivi sasa wengi wanatibiwa Zanzibar ambayo hayo ni mafanikio makubwa kwani lengo ni kuhakikisha wananchi wanatibiwa hapa ndani na kupunguza gharama pamoja na kujenga uwezo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment