WAZIRI wa Nishati Dk.Medard Kalemani amesema hali ya upatikanaji umeme kwa sasa nchini ni nzuri ambapo wana ziada kutosha.
Dk. Kalemani amesema hayo wakati wa semina iliyoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyohusisha wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo vya habari mbalimbali inayofanyika mkoani Morogoro.
“Tuna megawati 1,604 wakati matumizi ya Watanzania,ni megawati 1,180 hivyo zaidi ya megawati 400 ni ziada,” amesema.
Amesema hali halisi kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ni nzuri katika mabwawa yote saba ya kuzalisha umeme, kwa mfano bwawa la Mtera limejaa kufikia kikomo chake cha ujazo 698.76.
Amesema wanatarajia kulifungulia bwawa hilo hivi karibuni, kupunguza maji kwa lengo la kuilinda miundombinu.
“Bwawa la Kidatu limejaa kufikia mita za ujazo 448.81 wakati uwezo wake ni mita za ujazo 450,” ameongeza.
Akizungumzia Mradi wa Kuzalisha Umeme Julius Nyerere (JNHPP) Waziri Kalemani amesema unaendelea vizuri, kazi zote tano muhimu za ujenzi zinaendelea vyema na mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi trilioni 1.9 sawa na zaidi ya asilimia 100 aliyotakiwa kulipwa.
Amesema faida za mradi mbali na umeme wa uhakika, utasaidia kuokoa mazingira ikiwemo ukataji miti ambapo akitolea mfano Jijini Dar es Salaam magunia ya mkaa kati ya 400,000 mpaka 500,000 yanatumika.
Amesema JNHPP mpaka sasa imeshazalisha ajira zaidi ya 7,000 za moja kwa moja na zisizizo za moja kwa moja
Amesema ujenzi wa Mradi wa JNHPP unaenda sambamba na
kufunga minara ambapo hadi sasa wameshafunga minara 456 ya umeme na kipande cha Dar es Salaam hadi Kingolwira, kimekamilika kinachosubiriwa ni majaribio.
“Megawati 70 za umeme zimeshatengwa kwa ajili ya SGR hivyo hakuna cha kukwamisha mradi huo kwenye nishati hata kama ungeanza leo,” amesema Waziri Kalemani akizungumza na wahariri.
Aidha kuhusu usambazaji umeme vijiji kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), amesema hadi sasa vijiji 10,263 vimeshapata umeme kati ya vijiji 12,268 ambapo hadi 2024 vitakuwa vimepata umeme.
Kwa upende mwingine Dk.Kalemani amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeimarika kutoka kuendeshwa kwa hasara ambapo lilikuwa linapokea ruzuku ya shilingi bilioni 438 kutoka serikalini lakini tangu mwaka 2017,halipokei tena ruzuku.
“Limeondokana na hasara ya shilingi bilioni 478 toka mwaka 2017, kufuatia kuondokana na uendeshaji wa mashine za mafuta mazito na dharura, ikiwemo usitishaji wa mikataba na kampuni zikiwemo IPTL.
Aidha imeokoa hasara ya shilingi bilioni 720 kwa mwezi kufuatia kuondoa mashine za mafuta mazito na dharura katika mikoa 12 nchini.
Pia Kalemani alisema gesi asilia inazalisha asilimia 52 ya umeme wote unaotumika nchini.
“Pamoja na kuzalisha umeme, gesi asilia sasa inaunganishwa kwa matumizi ya nyumbani ambapo mpaka sasa jumla ya nyumba 3,000 zimeunganishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara pia magari 350 yameshaanza matumizi ya Gesi asilia badala ya Petroli na dizeli na kuokoa asilimia 45 ya matumizi ya bidhaa hizo za mafuta.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment