Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) imefanikiwa kuwadhibiti makundi ya nzige yaliyovamia wilaya za Longido na Simanjiro kwa kuwaua kwa kutumia ndege maalum iliyonyunyizia kiuatilifu kwenye maeneo ya mapori walipovamia.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (23.02.2021) katika kijiji cha Kimokouwa wilaya ya Longido wakati Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliopotembelea kukagua maeneo ambayo yalikuwa makazi ya nzige wa jangwani mara baada ya kazi ya upulizaji sumu uliofanywa na ndege maalum.
“Leo tumefanikiwa kuua makundi makubwa ya nzige wa jangwani kwenye wilaya za Simanjiro na Longido ambapo ndege maalum imefanya kazi hiyo asubuhi na hapa tunashuhudia tayari nzige wameanza kufa na hakuna nzige aliyepo angani hadi muda huu (saa 6 mchana) ninapozungumza nanyi waandishi wa habari hapa Longido” alisema Bashe.
Bashe alibainisha kuwa serikali mara baada ya kupata taarifa toka kwa wananchi kuwa eneo la wilaya ya Mwanga hapo mwezi Januari waliona nzige ilituma wataalam wa udhibiti wa visumbufu vya mimea toka TPRI kufuatilia nyendo zao na pia tarehe 16 Februari nzige wa jangwani waliingia Longido kupitia mpaka wa Namanga wakitokea Kenya hatua za mapema zilichukuliwa ili wasilete madhara.
Aliongeza kusema hadi nzige hawa wanaangamizwa leo hakuna eneo la kilimo ambalo mazao yake yameathirika na wadudu hao kutokana na hatua ambazo serikali kupitia wataalam wa wizara ya Kilimo imechukua.
“Hakuna eneo la kilimo ambalo limeathiriwa na nzige wa jangwani tangu waliporipotiwa kuingia nchini kwetu, hivyo wakulima na pia wafugaji wasiwe na hofu serikali ya awamu ya tano ipo madhubuti kuwakabiri ili nchi yetu iendelee kuwa na uhakika wa chakula” alisisitiza Naibu Waziri Bashe.
Katika hatua nyingine Bashe alitembelea na kujionea eneo la kilometa 39 za kijiji cha Kimokouwa wilaya ya Longido ambalo lilikuwa makazi ya nzige na kushuhudia makundi ya nzige yakiwa wamekufa na hakuna nzige aliyepo angani hatua inayoonesha ufanisi wa zoezi la kupulizia sumu.
Bashe aliagiza kuwa wataalam wa wizara kwa ushirikiano na mikoa yenye uvamizi wa nzige wataendelea kuwepo kwenye maeno yote ambayo nzige wamepuliziwa dawa kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kusitokee nzige wengine wakaendelea kusambaa.
“Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameagiza niendelee kubaki kwenye mikoa hii yenye uvamizi wa nzige kufuatilia kwa karibu hivyo kwa wataalam wote wanaohusika nanyi pia mtaendelea kubaki kwenye maeneo haya hadi serikali ijiridhishe na kutokuwepo kwa masalia ya nzige.” Alisema Bashe.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia za Unyunyiziaji na Udhibiti wa Visumbufu TPRI Mhandisi Julius Mkenda alisema ndege maalum imenyunyiza kiuatilifu(sumu) aina ya Fenitrothion 96% ULV chenye uwezo mkubwa kuua nzige wa jangwani ambapo eneo la hekta 412 za wilaya ya Longido ambako yalikuwa makazi ya nzige hao limefanikiwa kunyunyiziwa sumu hiyo.
“Tathmini ya awali leo asubuhi tumefanikiwa kunyunyiza sumu kwenye maeneo haya ya Kimokouwa na Ildoinyo kata ya Sinya wilaya ya Longido ambapo makundi ya nzige yalikuwa yamelala kisha ndege imefanikiwa pia kupuliza kiuatilifu maeneo ya Simanjiro na kazi imefanyika salama.” Alisema Mhandisi Mkenda
Mkenda aliongeza kusema kiuatilifu hicho kinafanya kazi kwa masaa kati ya 24 na 48 kuua nzige wote na kwa kuwa nzige hawa walikuwa bado wachanga kazi ya kuwaua itakauwa rahisi hivyo wataendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuona ufanisi wa zoezi hilo.
“Nzige hawa walikuwa bado wachanga hali inayosaidia kusiwe na hofu ya uwepo wa masalia baada ya kazi ya kuwapulizia leo. Tutaendelea kufuatilia maeneo yote walikopita kwenye vijiji kujua ufanisi wa kazi ya kuwadhibiti nzige “ alisema Mhandisi Mkenda.
Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya Visumbufu vya Mimea kutoka Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) Tanzania aliyeshiriki zoezi hilo Mushobozi Baitani alisema shirika hilo kazi yake ni kuhakikisha nchi wanachama zinakuwa na uhakika wa chakula kwa kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao ndio maana wameshirikiana na serikali kutafuta ndege maalum
Mushobozi aliongeza kusema baada ya uwepo wa taarifa za nzige kuingia Tanzania kutokea mpaka wa Kenya walianza jitihada za kutafuta viuatilifu na ndege ili kufanya kazi ya kudhibiti wasiongezeke na kufika mashambani .
“FAO muda wote tunashirikiana na serikali ya Tanzania kudhibiti majanga yanayohusu chakula na kilimo hivyo tatizo la nzige tumelikabili kwa pamoja ili uwepo uhakika wa chakula kwa wananchi wote” alisema Mushobozi
Mushobozi aliongeza kusema makundi makubwa ya nzige yapo kwenye nchi za Somalia, Kenya na Ethiopia ambapo kazi kya kuwadhiti inaendelea na kuwa ndege maalum iliyokuja Tanzania ikimaliza itarejea Kenya kwenda kufanya kazi ya kudhibiti mazalia ya nzige yasiweze kuenea kwenye nchi zingine inazopakana nazo.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Longido Joseph Ole Sadira akiongea kwa niaba ya wakulima alisema wanaishukuru serikali kwa kuchukua hatua za haraka kuleta ndege kudhibiti nzige waliokuwa wameanza kuongezeka kwenye maeneo ya wakulima na malisho ya wafugaji.
‘Tunaimani na serikali yetu kwa hatua za haraka ilizochukua kuwaua nzige hawa ambao wangeachwa wangeleta madhara kwa mazao ya kilimo na malisho ya mifugo yetu kwa kuwa Longido eneo kubwa ni la wafugaji hivyo tungekiosa nyasi” alisema Ole Sadira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Longido Jumaa Mhina alirejea agizo lake la kufungwa kwa shule za msingi na sekondari kwa siku 5 kwenye maeneo yote ambapo sumu imepuliziwa kuua nzige na kuwa watendaji wa vijiji na kata waendelee kutoa matangazo ili wananchi wachukue tahadhali.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment