Waziri Mkuuashiriki Mazishi Ya Dada Wa Spika Ndugai


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki mazishi ya dada wa Spika wa Bunge Job Ndugai, Mary Ndugai aliyefariki dunia Januari 23, 2021, wilayani Mpwapwa, Dodoma.

Mazishi hayo ya Mary Ndugai yamefanyika leo (Jumatatu, Januari 25, 2021) katika makaburi ya Ving’awe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Akizungumza baada ibada ya kumuombea marehemu Mary iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania jimbo la Mpwapwa, Waziri Mkuu amewaomba wafiwa wawe na subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu.

“Nimekuja kuungana nanyi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa Mheshimiwa Spika Job Ndugai kufuatia msiba mzito wa kuondokewa na dada yake mpendwa Mary.”

Waziri Mkuu amesema msiba huo ni mzito na jukumu kubwa ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pahala pema, hivyo amewaomba watoto wa marehemu, ndugu na jamaa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewashukuru viongozi wa dini, Serikali na waombolezaji kwa kujitokeza na kuifariji familia kufuatia msiba huo. Pia amewashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Mpwapwa ambapo marehemu alikuwa akitibiwa.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba, Katibu wa Bunge Stephen Kigaigai na baadhi ya wabunge.


 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments