Rais John Magufuli, amesema hatasita kuwaondoa mara moja wakuu wa wilaya zote ambao maeneo yao yatakumbwa na njaa mwaka huu.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yao kwa kulima mazao ya aina tofauti.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, akirejea kutoka kwenye ziara ya kikazi mikoa ya Geita, Shinyanga na Tabora.
“Hakuna chakula cha bure sitatoa chakula kwenye wilaya yeyote, wilaya itakayopata njaa, mkuu wa wilaya na yeye ataondoka pia na viongozi ambao wanazembea kuwahamasisha wananchi kufanyakazi.
Usiyefanya kazi usile, hakuna cha bure. Asiyefanya kazi na asile. Fedha tunayopata ikaendelee kujenga miradi ya SGR (Reli ya Kisasa),” alisema.
“Kazi ya serikali kujenga hospitali, kununua ndege, dawa, reli na mengine ya maendeleo. Kujilisha ni kazi yako, si kazi ya serikali,” alisema Rais Magufuli.
Alisema pamoja na kuona maeneo kadhaa ya wilayani humo, yakiendelea kuwa na mvua, hakuna kilimo kinachoendelea.
“Ukienda Morogoro utakuta kinamama wamepanga viazi. Bahi kuna mvua, lakini sioni mkilima. Nimeshangaa, mama wa miaka 59 anaomba ekari tatu, alime, nilidhani wakuniomba ni kijana wa miaka 18, tena mkampe kesho huyu mama.”
Kadhalika, akiwa eneo la Manyoni, mkoani Singida, Rais Magufuli aliwataka wananchi kulima ili kujiongezea kipato.
“Mvua hazina kusubiri, zinaonyesha tulime, barabara hizi zitaleta faida iwapo tutazifanyia kazi, mazao yenu yataliwa maeneo yote sababu barabara ipo,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema wakati mataifa mengine wananchi wao wakijifungia ndani kwa ajili ya corona, ni wakati wa Tanzania kufanya kilimo na kwamba viongozi wa eneo hilo wawahamasishe watu kufanya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dk. Fatuma Mganga, alisema mapato yameongezeka kutoka Sh. milioni 500 hadi Sh. bilioni moja.
Alisema ongezeko hilo limefanya ujenzi wa sekondari kwenye kata mbili ambako hazikuwapo awali, kujengwa.
“Kata ya Nondwa tayari watoto wanasoma na kata ya Mpinga tunamalizia madarasa, tunatarajia hadi Februari yatakuwa yamekamilika,” alisema Dk. Mganga.
Aliongeza kuwa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, yamewezesha kutoa mikopo kwa vikundi 33 na kutoa ajira kwa makundi maalum.
“Madarasa 12 yanajengwa kwa wanafunzi waliokosa ambao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza hadi mwezi ujao wataingia darasani.”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment