Katibu Mkuu Ndumbaro Awataka Watumishi Wa Umma Kuwahudumia Wananchi

 Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dr Laurean Ndumbaro amewataka watumishi wa Umma Nchini, kutoa Huduma Bora, na kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili ili wapate maendeleo.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki hii, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Nyasa katika Ukumbi wa Kapten John Komba,  alipofanya Ziara ya  Kikazi Wilayani Nyasa yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi Wilayani hapa.

Dkt Ndumbaro amefafanua kuwa, Serikali ya awamu ya Tano inawategemea sana watumishi wa Umma, katika kila eneo la utoaji Huduma, ili waweze kutoa huduma bora  kwa wananchi ambao kodi zao ndizo zinawalipa mishahara, hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa huduma bora ili waipende Serikali yao.

Amewaagiza watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa kila mtumishi kutokana na Taaluma yake kwa wakati, kwa lengo la kuwajibika na  kutatua kero za wananchi ili wananchi waweze kupata maendeleo.

“Napenda kuwakumbusha sisi ni Watumishi wa Umma, hivyo tuna kila sababu ya kuwapenda wananchi na kuwatumikia, na yeyote anayehitaji huduma katika Ofisi za Umma, apate huduma bora, na kila Mtumishi atoe Huduma, kulingana na Taaluma yake kwa kuwa wananchi hawa kodi zao wanazolipa, ndizo zinatulipa Mishahara. Aidha serikali ya awamu ya Tano imedhamiria Kutoa Huduma Bora kwa Wananchi hivyo kila Mtumishi wa Umma ajione analazimika kuwahudumia wananchi, na tunatakiwa kufahamu, sisi sio wafanyakazi wa Umma bali ni Watumishi wa Umma”.

Alisema, na kuwataka wakuu wa Idara na Vitengo kuwahudumia watumishi wanaofika kupata huduma katika Ofisi zao kwa haraka ili nao wakatoe huduma katika Sehemu zao za kazi kwa kuwahudumioa wananchi ipasavyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bw Jimson Mhagama amempongeza Katibu Mkuu wa huyo kwa kufanya Ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na kumuahidi yote aliyoyaagiza kama Mkuu wa Taasisi, atasimamia na kuhakikisha Watumishi wanawajibika ipasavyo ili kuwepo na Utawala bora na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.

Kero zilizotolewa na watumishi wa Wilaya ya Nyasa ni upandaji Madaraja, ulipwaji wa fedha za kujikimu wakati wa Uhamisho na Likizo.

Aidha Katibu Mkuu amezichukua kero hizo kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kuzitatua Changamoto hizo kwa kuwa Serikali inawajali watumishi wa Umma na wananchi kwa Ujumla.

Imeandaliwa na Netho C. Sichali

Afisa habari Wilaya ya Nyasa.


from MPEKUZI

Comments