Na. Edward Kondela
Serikali imesema itahakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinawaondoa wananchi katika umasikini, kupata ajira na nchi iweze kuuza bidhaa bora za mazao ya mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.
Akizungumza jana (28.12.2020) katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wakati akihitimisha ziara hiyo kwenye kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha Chobo kilichopo Kata ya Usagara Wilaya ya Misungwi amesema wizara imekuwa ikichukulia kwa uzito mkubwa suala la viwanda ambalo litaweza kubadilisha fikra za wafugaji na wavuvi.
“Wananchi wetu waondoe umasikini, wananchi wetu wapate ajira na sisi tuuze bidhaa za mazao haya ya mifugo na uvuvi yaliyo bora hapa ndani na kule kwa wenzetu nje, sasa mimi nikikuta hali ya mkwamo kwa kitu ambacho kinatusaidia kuelekea huko napata shida.” Amesema Mhe. Ndaki
Waziri Ndaki akifuatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul katika ziara hiyo amefafanua kuwa haridhishwi na baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wawekezaji ambao wamejikita katika kuyaongezea thamani mazao ya mifugo na uvuvi na kumuagiza Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Bw. Iman Sichalwe kumpatia taarifa ya hali ya viwanda vya nyama nchini ili apate tathmini halisi ya utendaji kazi wa viwanda hivyo, baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Chobo, Bw. John Chobo kubainisha baadhi ya changamoto ambazo Waziri Ndaki amesema wizara itahakikisha inafuatilia changamoto zinazoihusu wizara hiyo ili kuzipatia majibu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. John Chobo amesema kwa sasa kiwanda chake kimesimamisha uzalishaji na kinatarajia kuanza kurejea katika shughuli zake Mwezi Januari Mwaka 2021 baada ya ugonjwa wa Covid 19 kuathiri shughuli za kiwanda hicho ambacho kimekuwa kikisambaza nyama katika nchi za falme za kiarabu.
Bw. Chobo amesema kutopatikana kwa taarifa sahihi za mifugo kumekuwa kukichangia kwa kiasi kikubwa soko la nyama kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kuwekwa katika daraja la chini kwa kuwa mifugo mingi ambayo inachakatwa viwandani haina taarifa sahihi juu ya ukuaji wake, magonjwa na chanjo mbalimbali ambazo mfugo huo umepatiwa.
Akiwa katika Kiwanda cha kuchakata samaki Nile Perch kilichopo eneo la viwanda katika Kata ya Nyakato Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amewataka wawekezaji wa viwanda vya samaki vilivyopo Mkoani Mwanza kuhakikisha wanatumia usafiri wa ndege kutoka katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwanza kusafirisha minofu ya samaki ili kutangaza bidhaa zinazotengezwa hapa Tanzania.
“Tungependa kuona usafirishaji wa minofu ya samaki unafanyika hapa nchini kwetu, badala ya nchi jirani kwa kusafirisha kwa malori kwenda nchi za jirani, kuna uwekezekano kabisa wa kutoa minofu ya samaki kutoka kiwanja cha ndege cha Mwanza kwenda nje ya nchi badala ya kutumia nchi za jirani.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Aidha, amewataka wawekezaji wa viwanda vya samaki kuangalia namna ya kuongeza bei ya kununulia samaki kwa wavuvi wanaopeleka samaki katika viwanda hivyo ili wavuvi hao waweze kubadilisha maisha yao na kunufaika kupitia Sekta ya Uvuvi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo baada ya Meneja Mkuu wa Kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch Bw. Rupesh Mohan kumueleza Waziri Ndaki na Naibu Waziri Gekul kuwa viwanda vya samaki vimekuwa vikikosa malighafi ya kutosha kutokana na soko la ndani kukua na wakati mwingine kupata samaki kwa bei ya juu, hali iliyomlazimu Waziri Ndaki kubainisha kuwa kama bei ya soko la ndani imepanda ni dhahiri wavuvi watauza samaki katika soko hilo badala ya kupeleka viwandani ambapo wanauza kwa bei ndogo.
Hivyo amevitaka viwanda vya kuchakata samaki kuangalia upya bei ya samaki wanayonunua ili wavuvi nao waweze kunufaika na kuboresha maisha yao na viwanda pia viweze kupata malighafi za kutosha.
Pia, Waziri Ndaki ametembelea kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha Hong Lin International Ltd kilichopo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza na kufurahishwa na kiwanda hicho kwa kutumia kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwanza kusafirisha bidhaa zake kwenda nchi za nje.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bi. Wang Shenghong ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hali inayomuwezesha kufanya shughuli zake bila matatizo huku akiomba pia baadhi ya tozo zipunguzwe.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul wametembelea pia Maabara ya Taifa ya Uvuvi, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) na Kituo cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP).
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment