TSC: Hatuwaadhibu Walimu Ili Kuwakomoa Bali Kuwajenga Kimaadili


 Veronica Simba – TSC
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Moses Chitama ameitaka jamii kuelewa kwamba adhabu zinazotolewa kwa walimu wanaobainika kwenda kinyume na maadili hazilengi kuwakomoa bali zipo kisheria ili kuhakikisha nidhamu na maadili ya kada hiyo yanazingatiwa.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti hivi karibuni wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu nidhamu na maadili kwa walimu nchini.

Chitama alieleza kuwa, ualimu ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine hivyo ina miiko, taratibu na sheria zake zinazoiongoza na zinapokiukwa, Tume inawajibika kuchukua hatua ili kuhakikisha shule zinabaki kuwa mahala salama na sahihi kwa watoto wanaohusika.

“Ndiyo maana walimu hufundishwa tangu wakiwa vyuoni namna bora ya kuwalea watoto watakaokwenda kuwafundisha ili wawe raia wema katika jamii na Taifa kwa ujumla.”

Akizungumzia ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya walimu, Chitama alikiri kuwa tatizo hilo lipo na kuongeza kuwa changamoto ambayo imekithiri kwa sasa ni baadhi ya walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Alisema, Tume ya Utumishi wa Walimu, ambayo ni Mamlaka ya Nidhamu, imekuwa ikilikemea sana suala hilo na imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kulitatua ikiwemo kutoa semina za kuwajengea uelewa walimu na kwa wanaothibitika kutenda kosa hilo, hupewa adhabu ya kufukuzwa kazi.

Aidha, alitaja changamoto nyingine kuwa ni utoro kazini kwa baadhi ya walimu ambapo alibainisha kuwa uchunguzi uliofanywa na Tume umebaini kuwa baadhi ya wanaotoroka huenda kufanya kazi katika shule za binafsi huku wakiendelea kupokea mshahara wa serikali.

“Sasa kweli kwa hali kama hiyo ambapo wanafunzi wanakoseshwa haki yao ya msingi ya masomo na wengine kunyanyaswa kijinsia, unatarajia Tume ikae kimya tu? Ni lazima tuchukue hatua stahiki ili kukomesha hali hiyo,” alisisitiza Chitama.

Kwa upande mwingine, Kaimu Katibu huyo amewaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto badala ya kuwaachia walimu peke yao jukumu hilo.

Akifafanua, alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakikwepa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto kwa kisingizio cha kukosa muda kutokana na kazi wanazozifanya kujipatia kipato, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa watoto.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari walio kwenye utumishi wa umma, Tanzania Bara.

Imeundwa kwa Sheria Namba 25 ya mwaka 2015 na ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2016 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sharia na kanuni zake.


from MPEKUZI

Comments