Rais Dkt Magufuli Ashiriki Katika Misa Takatifu Ya Krisimasi Katika Kanisa La Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu


 Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli leo Disemba 25, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma kusali Misa Takatifu ya Krismasi ambayo ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Baada ya Misa hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza na kuwatakia heri Watanzania wote kwa sikukuu ya Krismasi na amewataka kuendelea kumshukuru Mungu kwa miujiza na upendo mkubwa anaolitendea Taifa la Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amesema upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa Corona (Covid-19) ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Amewaomba Watanzania wote waendelee kumshukuru na kumuomba Mungu aendelee kulilinda Taifa lao dhidi ya ugonjwa huo, na kuwaombea wananchi wa Mataifa mengine waepushwe na Corona.

Ametoa wito kwa viongozi wa Mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

Pamoja na kuwatakia heri ya Krismasi, Mhe.Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali ili kuendelea kujenga Taifa lao pamoja na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kila jambo.


from MPEKUZI

Comments