Na Shamimu Nyaki -WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia vyema Maadili na Utamaduni wa Taifa kupitia Sanaa ili kumuenzi aliyekua Katibu Mtendaji Marehemu Godfrey Mngereza.
Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Desemba 29, 2020 Jijini Dar es Salaam katika tukio la kuaga mwili wa aliyekua Katibu Mtendaji Marehemu Godfrey Mngereza ambapo amesema Serikali itaweka mazingira mazuri kwa nchi rafiki kwa ajili ya kupata soko la kuuza kazi za sanaa.
“Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 inaelekeza kusimamia vyema Sekta ya Sanaa na Michezo ambazo zinakua kwa kasi hapa nchini, na sisi kama viongozi tutaisimamia kikamilifu” Waziri Mhe. Bashungwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa wizara imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo, huku akieleza kuwa marehemu Mngereza alikua anasimamia Sheria pamoja kutenda haki kwa wadau wake. Na ni mtu ambaye waliheshimiana na kutaniana sana.
Naye waziri Mstaafu wa wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe ameleeza kuwa marehemu Mngereza alikua anaisimamia vizuri BASATA, hasa kukuza sanaa, kulinda utamaduni wa Taifa letu na kusimamia Sheria na taratibu za kufanya kazi ya Sanaa.
Aidha, Mbunge na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Humfrey Polepole amesema kuwa mazuri aliyoacha Marehemu Mngereza ni vizuri kuyaenzi na aliyoanzisha kuyaendeleze.
Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakari Kunenge alieleza masikitiko yake kwa kusema msiba hauzoeleki, huku akieleza kuwa jamii na wadau wa Sanaa wanapaswa kuendelea kumuenzi kwa kufanya mazuri kwakua kufanya hivyo atakua anaishi mioyoni mwao.
Halikadhalika, Msanii wa Kizazi Kipya Nasib Abdul (DiamondPlatnumz) alieleza kuwa marehemu Mngereza alikua mlezi mzuri kwa wasanii kupitia ushauri aliokua anatoa na pale palipohitaji ukali alitumia busara katika kufanya maamuzi.
Marehemu Godfrey Mngereza alifariki Desemba 24, katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na atazikwa Desemba 30, 2020 kijijini kwao Suji Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment