Tanzania Yaahidi Kuendelea Kuisaidia Congo Kulinda Amani Ukanda Wa Maziwa Makuu


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kuisaidia Congo kulinda amani na kuhakikisha changamoto za  ulinzi na usalama zinazoikabili nchi hiyo zinatatuliwa ili kuimarisha hali ya amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika kwa njia ya video (Video Conference).

"Tanzania tutaendelea kusaidia juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo la mashariki mwa Congo - DRC kwani kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama kwa nchi hiyo kunahatarisha usalama wa eneo lote la Jumuiya nzima ya ICGLR nayo itakuwa salama," amesema Prof. Kabudi.

Ameongeza kuwa Congo Brazaville ilikuwa ikikabiliwa na uasi kutoka kundi la Ninja lililokuwa  likiisumbua Serikali  kwa miaka mingi hata hivyo hadi kufikia katikati ya mwaka 2019 uasi ulitulia kufuatia mazungumzo ya kusitisha  mapigano kati ya kundi hilo na Serikali.

Amesema Congo-Kinshasa na Congo-Brazaville ni muhimu katika eneo la maziwa makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali za misitu, maji na madini ambavyo vinahitajika sana duniani na kuongeza kuwa umuhimu zaidi unahitajika kutokana na ukweli kuwa kuna haja kubwa ya kutunza mazingira, kuzalisha nishati na kukuza uchumi wa dunia.

"Nchi hizi mbili za DRC na Congo Brazaville ni nchi muhimu sana katika eneo la Maziwa Makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali, baadhi ya rasilimali hizo kama misitu, maji na madini zinahitajika sana duniani kwa sasa kutokana na umuhimu wake, umuhimu ambao unatokana na haja ya kutunza na  kulinda mazingira, uzalishaji wa nishati na kukuza uchumi wa dunia," alisema n kuongeza kuwa Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama katika nchi hizi kunahatarisha usalama wa eneo lote la Maziwa Makuu ikiwemo na usalama wa dunia kutokana na uwezekano wa baadhi ya mataifa makubwa kugombea rasilimali hizo", alisisitiza Prof. Kabudi.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya ICGLR umepokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu Jumuiya hiyo , mbali na hali ya kisiasa na kiusalama katika Ukanda huo umeangalia pia suala la michango ya wanachama katika bajeti ya Sekretariat na Mfuko Maalum wa maendeleo, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi  kuhusu hali ya usalama wa Ukanda wa Maziwa Makuu na taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Afya.

Nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Kati, Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

Oktoba 2019, Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulifanyika nchini Congo Brazzaville.

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kumuaga Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Bw. Alex Mubiru ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru Bw. Mubiru kwa mema aliyoyafanya hapa nchini hasa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua kimaendeleo.


from MPEKUZI

Comments