Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Aanza Kutekeleza Agizo La Rais Magufuli Kuhusu Biashara Ya Mazao Ya Kilimo Nje Ya Nchi


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya leo mchana tarehe 27 Novemba, 2020 ameanza kutekeleza agizo la Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuwataka Watendaji wa Wizara ya Kilimo kuendelea kujenga mazingira bora na wezeshi ya biashara ya mazao ya kilimo kwenda nje ya nchi kama alivyohutubia wakati wa kufungua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba, 2020.

Katika kulitekeleza agizo hilo Katibu Mkuu Kusaya amewatunuku vyeti Wakaguzi wa Ubora wa Mazao ya kilimo na Afya ya Mimea 32 kutoka Vituo vya ukaguzi vya mipakani na viwanja vya ndege vya Wizara ya Kilimo katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.

Katika hotuba yake hiyo; Rais John Pombe Magufuli alisema Serikali katika kipindi cha miaka hii mitano; Itanunua ndege ya kusafirisha mazao ya kilimo na itaboresha mazingira ya Sekta Binafsi kufanya biashara ya mazao ya kilimo kama mbogamboga, matunda, maua na viungo ambayo katika mwaka uliopita yaliingizia taifa fedha za kigeni kiasi cha dola milioni 779.

Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali itanunua ndege maalum kwa ajili ya kusafirisha mazao ya kilimo pamoja na bidhaa nyingine kwenda nje ya nchi kuongeza kuwa Watendaji wa Wizara ya Kilimo, Biashara, Mambo ya Nje na Mabalozi wajipange vizuri kwa ajili ya kufanikisha jambo.

Katibu Mkuu Kusaya amesema wakati akiwatunuku vyeti Wakaguzi hao baada ya kupata mafunzo ya wiki moja; Lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Wakaguzi wa Afya ya Mimea, mbinu mpya za ukaguzi katika mazingira ya sasa pamoja na kutimiza takwa la kisheria ambalo; Linawataka Wakaguzi wa Afya Mimea kutoka Vituo vyote nchini kupewa mafunzo ya mara kwa mara kwenye eneo la ukaguzi wa mimea wakati wanapotimiza majukumu yao ya kila siku.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikiajiri Wakaguzi hao na kwa kipindi kifupi Wakaguzi hao walikuwa hawajajengewa uwezo wa namna bora ili kuwawezesha kuwa na mbinu zinazoendana na mahitaji ya nyakati hizi katika shughuli zao za ukaguzi na pia kabla ya kutangazwa kwenye GAZETI LA SERIKALI.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yalilenga kuwafundisha Wakaguzi hao kuhusu mikataba ya usafi wa mazao kulingana na viwango vya ubora wa kimataifa sawa sawa na taratibu za Kimataifa zinavyotaka ili Wanyabiashara wa Tanzania waendelee kuuza mazao ya kilimo (Mbogamboga, matunda, maua na viungo) kwenda nje ya nchi ili kuongeza mapato mara mbili ya mwaka 2018/2019; Mapato ya dola za Marekani milioni 779.

“Napenda mfahamu kuwa Wakaguzi wa Afya ya Mimea mnafanya kazi ya muhimu kwa Taifa letu, shughuli yenu ni ya kisayansi lakini pia ni ya ulinzi na mahusiano kimataifa; Nitahakikisha mafunzo haya yawe yanatolewa kila baada ya miezi sita kwa kuwa kila siku mambo yanabadirika, napenda na sisi tuwe tunaongeza ujuzi mara kwa mara”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu ameongeza kuwa mbali na mafunzo hayo; Wakaguzi hao pia walifundishwa kuhusu usimamizi na ufukiziaji viuatilifu kwa mazao yanayoingia na yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi, Mfumo wa ATMIS ambao unatoa vibali vya usafi wa mazao yanatoka au kuingia nchini.

“Ninaamini baada ya mafunzo haya; Wakaguzi mtafanya kazi zenu kwa ufanisi mkubwa. Nitatembelea Vituo vyenu, nataraji kuwaona mkifanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Mafunzo haya mliyoyapata yasiishie hapa hapa katika majengo cha Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) tu bali yakawe chachu ya kujenga uchumi wa nchi kupitia ninyi”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

“Wakaguzi wetu wa Afya ya Mimea fanyeni kazi kwa ukaribu na Sekta Binafsi wakiwemo Wakulima na Wasafirishaji wa mazao ya kilimo kwenda nje ya nchi au kuingia nchi; Uchumi unajengwa na mahusiano mazuri kwanza na kujua changamoto zao”.

“Serikali tutaendelea kujenga mazingira wezeshi ya Sekta Binafsi kufanya biashara kwa tija na ufanisi mkubwa.” Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya

Napenda niwakumbushe kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati akizindua Bunge la 12; Katika hotuba yake ameahidi katika kipindi cha miaka mitano hii; Serikali itanunua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha uzafirishaji wa mazao ya bustani. Wakulima wetu ni lazima watajirike kutokana na shughuli wanazozifanya; Tunapaswa kutoa huduma bora kwa Sekta Binafsi wakiwemo Wakulima, Wafanyabiashara ya mazao ya bustani (Mbogamboga, matunda maua na viungo) na Wafanyiashara kutoka nje ya Tanzania.

“Uelewa wa wakaguzi katika masuala afya ya mimea na viuatilifu ni fursa muhimu katika kulinda ustawi wa kilimo, maliasili, mazingira na afya ya binadamu dhidi ya madhara yatokanayo na visumbufu na viuatilifu hatarishi”.

“Wizara ya Kilimo itaendelea kutoa mafunzo ambayo yatalenga kuimarisha  usimamizi wa masuala ya  afya ya mimea na viuatilifu na hivyo kuimarisha uhakika wa chakula na kuboresha fursa za biashara.” Amemalizia Katibu Mkuu. 



from MPEKUZI

Comments