Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Halmashauri 45 ambazo hazijaunda kamati za watu wenye ulemavu kutoa maelezo ndani ya siku tano.
Akifungua Mkutano wa wadau wa Chama cha Wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi jana amesema hadi sasa halmashauri 140 zimeunda kamati hizo lakini nyingine bado hazijafanya hivyo, jambo ambalo linarudisha nyuma mikakati ya Serikali ya kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Amesema kamati hizo ni muhimu kuundwa kwa kuwa zinarahisha mawasiliano kati ya jamii ya watu wenye ulemavu na serikali na kuweka mikakati bora ya jinsi ya kutatua changamoto zao wanazozipitia katika jamii kwa haraka.
“Kwa halmashauri ambazo hazijaunda kamati hizo natoa siku tano kutoa maelezo wanataka nini ili waunde kamati hizo,waliambiwa mwaka gani na sababu za kutokuunda kamati ni nini na wana mikakati gani ya kuanzisha kamati hizo”, ameagiza Dkt. Gwajima.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kuwa kutokuundwa kwa kamati hizo kumesababisha kukata mawasiliano kati ya jamii ya watu wenye ulemavu na Serikali katika suala zima la utoaji wa huduma za afya kwa jamii kwa kuwa lengo la serikali ni kuwafikia watu wenye uhitaji.
Aidha Dkt. Gwajima amewataka wadau mbalimbali nchini kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kabla ya Ujauzito ili kupunguza tatizo la watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa nchini.
Dkt. Gwajima amesema kuwa kuna umuhimu wa kuweka mikakati itakayosaidia kutoa elimu kuanzia ngazi ya chini ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa jamii, jambo ambalo litasaidia kumaliza au kupumguza kabisa tatizo la kupata watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.
Dkt. Gwajima amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa kujenga na kukarabati vituo vya afya nchini na kupeleka vifaa tiba kwa lengo la kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa wananchi.
Hivyo Dkt.Gwajima ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatumia vituo vya afya hasa kwa wale watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.
Pia ameitaka jamii kuacha mila potofu za kuamini kuwa mtoto anapozaliwa na tatizo la Mgongo wazi na kichwa kikubwa kuwa wamelogwa hivyo kupelekea baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wao jambo ambalo linasababisha ucheleweshwa kwa matibabu ambayo yangemsaidia kupona kwa haraka.
“Jamii ielimishwe kuhusu chanzo cha kuzaliwa kwa watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa ili waondokane na dhana potofu walizonazo ili kuwaokoa watoto wenye tatizo hilo na jinsi ya kukabiliana nalo” amesisitiza Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima ameagiza wadau wote kuhakikisha wanatoa elimu kwa kamati za vituo vya afya nchini kwa kuwa zina wananchi ambao ni wajumbe ili wajue takwimu sahihi ya watoto wenye vichwa vikubwa.
“Wekeni mikakati ya kutumia mifumo ya afya iliyopo katika jamii ili kupunguza watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi katika jamii yetu”, ameeleza Dkt. Gwajima.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment