Watu 13 Wafariki kwa Ajali, Ngara – Kagera Baada ya Basi la Emirates Kupinduka


Watu  13 wamefariki dunia na wengine 11 wamejeruhiwa mkoani Kagera kufuatia ajali ya basi la Emirates ambalo hufanya safari zake kati ya Ngara na Mwanza.

Ajali hiyo imetokea baada ya basi hilo kuanguka na majeruhi wamelazwa Hospitali Teule ya Nyamiaga wilayani Ngara leo Jumamosi, Oktoba 24, 2020.

Mkuu wa wilaya Ngara, Michael Mntenjele, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema: “Ni kweli ajali hiyo imetokea mbele kidogo kutoka hapa Ngara mjini..Eneo la tukio kuna mteremko mkali, huenda gari lilimshinda breki, kwa hiyo akawa amepata ajali na kuanguka upande wa mteremko.

“Watu 13 wameshathibitika kupoteza maisha mpaka sasa wakiwemo wanaume watu wazima saba, wanawake watu wazima watatu na watoto watatu, pia kuna majeruhi 11 akiwemo dereva wa gari hilo ambao bado wapo hospitali wanaendelea na matibabu.  Hali zao siyo nzuri sana kutokana na ajali yenyewe ilivyokuwa mbaya sana ambapo kipande cha juu cha gari chote kimeondoka,” amesema Mntenjele.


from MPEKUZI

Comments