Mwambe, Katani Waeleza Machungu Ya Upinzani


 WAGOMBEA UBUNGE wawili wa Mkoa wa Mtwara waliotoka vyama vya upinzani na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) wameeleza machungu waliyokuwa wakikumbana nayo wakati wakitaka kuwatumikia wananchi wao.

Wabunge hao Bw. Cecil Mwambe (Ndanda) na Bw. Katani Ahmed Katani (Tandahimba) ambao wamehamia CCM kwenye kinyang’anyiro hiki cha ubunge, wamewaonya wakazi wa Masasi wasifanye makosa ya kuchagua wagombea wa upinzani kwani wataendelea kukosa maendeleo.

Wametoa wito huo jana (Jumatano, Oktoba 21, 2020) kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa CCM uliofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba kata ya Mkuti, wilayani Masasi, mkoani Mtwara ambako Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Bw. Mwambe anayegombea Ndanda na ambaye alihamia CCM akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema licha ya kuwa alikuwa akitamani wananchi wake wapate huduma muhimu kama maji, afya na barabara, haikuwa rahisi kwake kuchangia bajeti ya maendeleo kwa sababu walikuwa wanakatazwa.

“Mambo yaliyokuwa yanafanyika huku Masasi hata sisi kule Ndanda tulikuwa tunayatamani. Hii ni kwa sababu hakuna cha maana kule kilichoandikwa kwa ajili yenu, na mimi ni shahidi. Katika miaka mitano ya ubunge wangu, sijawahi kuitikia NDIYO na madhara yake nimeyaona. Ninawaomba sana, msifanye makosa hayo,” alisema.

Naye Bw. Katani anayegombea Tandahimba na ambaye alihamia CCM akitokea Chama cha Wananchi (CUF), aliwataka wananchi hao wasifanye makosa kwa sababu kule alikokuwa hawana ilani.

“Kama Katani anayeongea hapa mbele yenu, alikuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa na kaikimbia CUF, wewe ni nani mwananchi wa Masasi hata upinge maendeleo ya nchi hii? Tena niwaambie, kule hakuna ilani. Nawaomba wana Masasi msifanye makosa ya kuchagua wagombea wa upinzani, sisi wenzenu tumeyaona tukiwa Bungeni.”

“Ukienda Bungeni kutaka kusema Masasi tuna shida ya umeme, wakubwa wanasema kapinge bajeti. Tutaupataje umeme? Tumekwenda Bungeni tumepiga plasta, sasa ukitaka kuomba umeme, utaongea vipi na wewe midomo umeifunga plasta?”

“Wana Masasi msitucheleweshe, hii gari ya Dkt. Magufuli inatelemka kwa kasi kuleta maendeleo huku mikoa ya Kusini. Acheni Geofrey Mwambe awe mbunge wa jimbo la Masasi, alete maendeleo,” alisisitiza.

Wakati huohuo, mwanasiasa mkongwe na Waziri Mstaafu, Mama Anna Abdallah alisema anashangazwa na tabia ya mgombea urais ambaye anatangaza kwamba ndoa za jinsia moja ni haki ya msingi ya wananchi.

“Yuko mgombea wa urais ambaye yeye anasema haonei aibu ushoga eti anauunga mkono. Yaani mwanaume amuoe mwanaume mwenzake na mwanamke amuoe mwanamke mwenzake.”

“Anasema eti ni haki za binadamu. Hivi kama baba yake angemuoa mwanaume mwenzake au mama yake angeolewa na mwanamke mwenzake, yeye leo angekuwepo na angekuja kugombea urais?”

“Rais wa namna hiyo ana mawazo ya kishetani, hakuna dini hata moja inayosema juu ya ushoga. Hata wanaogombea kwa kupitia chama hicho ninaanza kuwatilia shaka. Hakuna ushoga katika nchi hii, hatutakiii! Haiwezekani, sisi tulioko hapa tumezaliwa na sisi tumezaa. Watoto wetu waache kuzaa kwa ajili ya mtu mmoja anayesema hiyo ndiyo haki. Hakuna haki kwenye ushoga, ni dhambi,” alisisitiza.

Mapema, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Masasi, Bw. Rashid Chuachua alisema katika wilaya hiyo, ndani ya miaka mitano, waliwezaa kujenga madarasa 108 ya shule za sekondari na mengine 355 ya shule za misngi.

Alisema kiasi cha sh. bilioni 3.5 kilitolewa kwa ajili ya elimumsingi bila malipo huku sekta ya afya ikiboreshwa kwa kujenga kituo cha afya cha Mbonde kwa gharama ya sh. milioni 500 na hospitali ya Mkomaindo ikipatiwa jengo la upasuaji lililogharimu sh. milioni 228.

“Mradi wa maji unaendelea kujengwa na ukikamilika, hatutakuwa na shida kabisa ya maji hapa Masasi,” alisema na kuwaombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Masasi, Bw. Geofrey Mwambe; na wagombea udiwani 14 wa CCM wa jimbo la Masasi.

(mwisho)


from MPEKUZI

Comments