Dr Mwinyi Ashinda Urais Zanzibar kwa Asilimia 76

 


Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imemtangaza mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi kuwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote.

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahamoud Hamid amesema  wagombea urais walikuwa 17 waliopigiwa kura  498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha.

Amesema kura zilizoharibika zilikuwa 10,944 sawa na asilimia 2.19.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 96 (2 na 3) ya Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya 2018, namtangaza rasmi Dk Hussein Ally Mwinyi wa CCM kuwa amechaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020,” amesema.

Jaji Hamid amesema ZEC imehakiki matokeo ya wagombea wote wa Zanzibar na kujiridhisha kuwa yako sahihi.

Amesema mgombea anayefuatia ni Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

.


from MPEKUZI

Comments