Wizara Kuweka Kipaumbele Cha Ajira Za Wauguzi Nchini

Na.WAMJW-Manyara
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua upungufu uliopo wa  wauguzi kwenye hospitali za rufaa za mikoa nchini na hivyo kuweka kama kipaumbele kwenye ajira Serikalini.
 
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya afya Bi. Ziada Sellah wakati akiongea na wauguzi na wakunga kwenye Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara.
 
“Tayari wizara inatambua upungufu huo na kwamba ajira zitakapotoka vipaumbele vitakuwa ni kuongeza waguzi hospitalini  hapo” Alisema Bi. Ziada.
 
Licha ya upungufu wa wauguzi katika hospitali hiyo Mkurugenzi huyo pia amewataka wauguzi hospitalini hapo kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa, ili wagonjwa  waweze kupata ahueni kwa kupatiwa huduma nzuri kutoka kwa wauguzi.
 
Aliongeza kuwa kila muuguzi nchini akumbuke kiapo alichokiweka kwa kuzingatia maadili na miiko ya muuguzi katika kumuhudumia mteja wake
 
Imetajwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara  inakabiliwa na upungufu wa  wauguzi 200. Upungufu huu ni zaidi ya asilimia 60% ya mahitaji.
 
Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga yupo kwenye ziara ya kikazi ya kukagua huduma za Uuguzi katika hospitali za Rufaa za mkoa ya Singida,Manyara,Arusha, Kilimanjaro na Arusha pamoja na hospitali maalum na kanda ili kusikiliza changamoto zinazoikabili kada hiyo ya wauguzi na kuzipatia ufumbuzi ili wauguzi waweze kufanya kazi zao katika mazingira rafiki.


from MPEKUZI

Comments