MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewapokea wanachama 20 kutoka Chama cha Demokrasia (CHADEMA) ambao wameamua kurudi CCM.
Wanachama hao wameongozwa na Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera, Bw. Francis Mutachunzibwa ambaye pia alimtambulisha Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA, Bi. Getrude Ndibalema ambaye alijiuzulu uongozi tangu mwaka jana.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Mutachunzibwa alisema: “Ninaijua vizuri CHADEMA, nilipotea, nilitenda dhambi lakini sasa nimeamua kurudi nyumbani, nipokeeni.”
“Ninawaomba wana-Bukoba tumchague Dkt. Magufuli, mashine ya kusaga na kukoboa, jembe la nguvu. Kuanzia kesho, nitamnadi yeye na Advocate Byabato hadi kieleweke.”
Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba leo jioni (Jumatatu, Septemba 28, 2020) waliojitokeza kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wakazi hao wajitafakari sana wanapofikiria kumchangua mtu wa kuongoza nchi.
“Tunataka kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ili umpate ni lazima umjue historia yake. Kuongoza nchi si lelemama, kiongozi wa nchi ni Mkuu wa Nchi, tena ni Mkuu wa Majeshi.”
Mheshimiwa Majaliwa ambaye ameanza ziara katika mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Wakili Steven Byabato, mgombea udiwani wa kata ya Bilele, Bw. Tawfiq Sharif Salum na madiwani wengine wa jimbo hilo.
Aliwasimamisha wazee wa Kagera wakiwemo aliyekuwa Meya wa Bukoba, Dkt. Anatoly Amani, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki ambao wote waliomba kura za Dkt. Magufuli, Wakili Byabato na madiwani wa jimbo hilo.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Bw. Charles Mwijage, alisema Muleba wana ajenda ya kuhakikisha kura zote zinaenda kwa Dkt. Magufuli na wabunge wa CCM na akawataka wana-Bukoba nao wafanye hivyo ili kuhakikisha majimbo yote tisa yanabakia CCM na pia wanapata wabunge wanne wa viti maalum.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment