Wakazi 60,000 Babati Kupata Majisafi Na Salama


Jumla ya wakazi 60,000 wa Mji wa Magugu Wilayani Babati Mkoani Manyara wanatarajia kunufaika na huduma ya maji pindi mradi wa maji unaotekelezwa kwa kutumia chanzo cha Mto Kou utakapokamilika.

Hayo yameelezwa Septemba 27, 2020 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wilayani humo ya kukagua hatua ya utekelezaji wa mradi huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA), Mhandisi Idd Msuya.

Mara baada ya kupokea taarifa na kujionea hali halisi ya hatua iliyofikiwa ya utekelezwaji wa mradi, Mhandisi Sanga aliielekeza BAWASA kufanya mapitio ya mradi kwenye baadhi ya maeneo ili kuongeza tija.

“Hakikisheni mtandao wa maji unaongezeka ili muweze kuwafikia wananchi wengi zaidi lakini pia wananchi waweze kunufaika kwa Saa 24 kila siku,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Aidha, Katibu Mkuu Sanga aliielekeza BAWASA kuhakikisha mradi huo wa Magugu unakamilika kwa wakati na kwamba jitihada zifanyike ili utekelezwaji wake ufanyike bila kusimama.

“Inatakiwa muongeze watendaji zaidi kwa ajili ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa muda uliopangwa; hakuna sababu ya kuchelewesha mradi,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Katibu Mkuu Sanga alitembelea eneo la mradi ambapo alikagua ujenzi wa mitambo ya kuchuja maji pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji kwenye Mto Kou.

Mradi wa maji katika mji wa Magugu unatekelezwa na Wizara ya Maji kwa gharama ya Shilingi Milioni 575 kupitia Mamlaka ya Maji Babati kwa lengo la kuongeza hali ya upatikanaji wa maji pamoja na kuboresha ubora wa maji yanayotumika kwa sasa.

Kwa mujibu wa Mhandisi Msuya, mradi unatekelezwa na wataalam wa BAWASA na kwamba ulianza kutekelezwa rasmi Agosti 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2020.

Katibu Mkuu Sanga amekamilisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maji Wilayani Babati


from MPEKUZI

Comments