MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imeimarisha miundombinu ya usafiri nchini ili wananchi waweze kuchagua aina ya usafiri wanaotaka pindi wanapotaka kusafiri.
"Tunataka tuhakikishe Watanzania wanatumia njia zote za usafiri kulingana na matakwa yake ndio maana tunatengeneza barabara, tumenunua ndege, tunajenga reli pamoja na kuendelea kuboresha usafiri wa majini," amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Misungwi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Amani wilayani humo, mkoani Mwanza.
"Tunajenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Dodoma, baadaye itatengenezwa ifike hadi Tabora na Mwanza. Ukitaka kupanda ndege una uhuru, ukitaka treni nenda, ukitaka basi, barabara nzuri zipo na ukienda majini nako pia tumeboresha usafiri,” amesema.
Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Aliwasisitiza wakazi hao wasiache kupiga kura siku hiyo. Mbunge wa jimbo la Misungwi, Bw. Alexander Mnyeti na madiwani wote 27 wa jimbo hilo wamepita bila kupingwa.
“Tunataka tuwe na kiongozi ambaye anaweza kuratibu maendeleo ya Watanzania, kiongozi ambaye anaweza kurudi chini na kujua kuna changamoto gani, tunataka kiongozi ambaye ana uwezo wa kusimamia rasilimali zetu, na huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli,” amesema.
Akielezea sekta ya mifugo, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Rais wetu amefanya maboresho makubwa sana katika sekta ya mifugo, Rais anataka kuona wafugaji na wavuvi wananufaika na shughuli zao, yale mapori makubwa tunachukua ili wafugaji wapate sehemu za malisho pia tunajenga mabwawa hukohuko, tunajenga maabara kwa ajili ya kutibu mifugo yetu. Kwenye uvuvi tunaimarisha sekta hiyo, ili kuhakikisha tunaendelea kuinua sekta hiyo, tumepunguza kodi pamoja na kuondoa tozo mbalimbali.”
(mwisho)
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment