Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2020 ni wa sita tangu chaguzi za vyama vingi kuanza nchini Tanzania, ukitanguliwa na chaguzi kama hizo mwaka 1995, 2000, 2005, 2010, na 2015. Katika chaguzi zote zilizopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliongoza kwenye nafasi ya urais katika pande zote mbili yaani Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Katika uchaguzi wa kwanza uliovishirikisha vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, mshindi alikuwa ni hayati Benjamini Mkapa ambaye aliibuka na ushindi wa asilimia 61.8 na alishinda tena mwaka 2000 kwa asilimia71.7.
Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80.28 mwaka 2005 na kushinda tena uchaguzi wa mwaka 2010 kwa asilimia 62.8, na mwaka 2015 John Pombe Magufuli alishinda urais wa Muungano kwa asilimia 58.46.
Hata hivyo uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa na ushindani mkubwa zaidi kwa upande wa urais ambapo baadhi ya wagombea wa urais kupitia vyama mbalimbali vya siasa vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), na chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) wamesimamishwa na vyama vyao kugombea nafasi hiyo kwa ajili ya kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wakati huu nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu, utakaofanyika tarehe 28, Oktoba, 2020, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ina jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa mchakato mzima wa uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba kwa kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi watakao waongoza katika miaka mitano ijayo
Aidha sambamba na utoaji wa wa elimu ya mpiga kura Tume imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali juu ya makosa ya uchaguzi na maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Makosa hayo yanaweza kufanywa na wapiga kura ambao ni wananchi au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kujiandikisha zaidi ya mara moja, kujaribu kupiga kura zaidi ya moja katika uchaguzi, kujaribu kupiga kura kwa kutumia kadi ya mtu mwingine, kujaribu kupiga kura wakati huruhusiwi kisheria kupiga kura na kuchana orodha ya wapiga kura au mabango yoyote ya elimu kwa mpiga kura yaliyopo vituoni.
Makosa mengine ambayo yameainishwa na NEC ni pamoja na kughushi, kuharibu au kuchafua kadi ya mpiga kura, kuwa au kumiliki kadi ya mtu mwingine na kuzembea kuirudisha kwa mwenyewe au Msimamizi wa Uchaguzi, kushawishi au kumsababishia mtu mwingine kujitoa kuwa mgombea kwa ukuwadi au ahadi ya malipo pamoja na kutoa hongo au takrima.
Vitendo hivi vinaweza kusababisha ukosekanaji wa haki hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 94 sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 inaelezea adhabu ya makosa ya utoaji hongo/takrima kuwa ni faini isiyopungua shilingi laki moja au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja
Kwa upande wa kutangaza matokeo ya uchaguzi, kifungu cha 81 cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 82 cha sheria ya Uchaguzi ya Serikari za Mitaa sura ya 292 mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi ni msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, hivyo basi ni kosa kutoa siri yoyote inayohusu mgombea au mchakato wowote unaoendelea katika kituo cha kupigia kura.
Lengo la sheria hii ni kuhakikisha kuwa utangazaji na utoaji wa taarifa yoyote ya uchaguzi unafanywa na watu waliopewa idhini kwa mujibu wa sheria. Mtu atakayekutwa na kosa hili atapata adhabu ya faini isiyopungua shilingi laki moja na isiyozidi laki tatu au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi kumi au vyote kwa pamoja hii ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya taifa ya uchaguzi, sura ya 343.
Wananchi na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wanapaswa kuyafahamu na kuyaepuka makosa haya ya uchaguzi ambayo yanaweza kusababisha kupotea kwa haki, kuleta migogoro katika kipindi cha uchaguzi lakini pia kupoteza demokrasia ya nchi yetu hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika uchaguzi mkuu.
Baadhi ya vyama vinavoshiriki katika uchaguzi wa mwaka huu ni pamoja na CCM, CHADEMA, CUF, ADC, Union for Multparty Democracy (UMD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP),NCCR-MAGEUZI, Tanzania Labour Party (TLP),CHAUMA, Sauti ya Umma (SAU) na ACT- Wazalendo.
NEC inawahimiza Watanzania wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa kufika katika vituo walipojiandikisha siku ya Jumatano, tarehe 25 Oktoba, na kuweza kuwachagua viongozi wao watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Kura zitakazopigwa ni kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment