Mbunge mteule wa Jimbo la Babati Mjini (CCM) Paulina Gekul ameahidi kuzibeba kero za wananchi wa jimbo hilo na kuwasilisha serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ametoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiongozi kata ya Maisaka, Kijiji cha Chemchem kata ya Mutuka pamoja na Balowa Kata Nangara kwenye mikutano ya kampeni za Chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais Oktoba 28 mwaka huu.
Amewaomba Wananchi katika Jimbo la Babati Mjini, wajitokeze kukipigia kura Chama cha Mapinduzi kumchagua Rais Magufuli na Madiwani wanaotokana na chama hicho ili kuendelea kuwahudumia wananchi katika kipindi Kingine cha Miaka Mitano.
Mbunge huyo anaesubiri kuapishwa, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kiongozi kata ya Maisaka, ameahidi kutafuta Suluhu ya mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kijiji hicho na wamiliki wa shamba la Tinna Estate.
Aidha ameahidi kuendelea kushirikiana na Viongozi wa chama na serikali katika kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Elizabeth Malle amesema kwa mambo mengi ya maendeleo aliyoyafanya Rais Magufuli na kuwasikiliza wanyonge, anastahili kupewa kura nyingi katika uchaguzi huo ili aendelee kuongoza Watanzania.
Mgombea Udiwani kata ya Mutuka Yona Wawo amesema katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo atahahakikisha anashirikiana na Mbunge ili shule shikizi iliyopo katika kijiji cha Chemchem inapata usajili na kuwa shule inayojitegemea ili wanafunzi wasiende Umbali Mrefu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment