Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa onyo kwa vyama vya siasa kwa kukiuka masharti ya kisheria kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katika barua yake kuhusu hadhari hiyo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, amewakumbusha wagombea wa vyama vya siasa kuzingatia masharti ya sheria katika kampeni hizo.
Kwa mujibu wa barua ya msajili huyo kwenda kwa makatibu wa vyama vyenye usajili wa kudumu iliyoandikwa Septemba 18, mwaka huu, vyama hivyo pia vimekumbushwa kufuata sheria katika kile kinachoitwa kuungana kwenye uchaguzi.
Alisema katika mikutano ya kampeni, baadhi ya wagombea wameonekana na kusikika wakiwaombea kura wagombea wa chama kingine cha siasa, akisisitiza kuwa sheria imeweka utaratibu wa vyama vya siasa kushirikiana katika uchaguzi.
Alivikumbusha vyama hivyo kuwa wajibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ni kuchukua hatua za kisheria dhidi ya chama cha siasa kinapokiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Msajili wa Vyama vya Siasa hatasita kuchukua hatua stahiki za kisheria pale itakapothibitika chama cha siasa kimekiuka sheria hizo,” alisema Nyahoza.
Ingawa Nyahoza hakutaja majina ya vyama vya siasa vilivyoingia katika hatari hiyo ya kukumbana na rungu lao, baadhi ya vyama vimeshaweka wazi kushirikiana na wagombea wa vyama vingine katika uchaguzi huo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akiwa visiwani Zanzibar kuzindua kampeni kanda, alitangaza chama hicho kitamuunga mkono mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT- Wazalengo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Pia, hivi karibuni, Maalim Seif katika moja ya mikutano yake ya kampeni visiwani huko, alitangaza kuwa atamuunga mkono mgombea urais wa Tanzania Bara kwa tiketi ya CHADEMA, Lissu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment