TCRA Yaifungia Clouds TV na redio kwa Siku 7

Mamlaka  ya Mwasiliano Tanzania (TCRA) imeagiza Clouds TV na Redio kusitisha matangazo yao kwa muda wa siku saba kuanzia kesho Ijumaa 28 Agosti hadi 3 Septemba 2020 kwa kosa la kukiuka kanuni za utangazaji na kanuni ndogo za utangazaji za uchaguzi.

Pia, mamlaka hiyo imevitaka Clouds TV na Redio kuomba radhi siku nzima ya leo Alhamisi tarehe 27 Agosti 2020 kwa kosa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari makamo makuu ya mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba amesema, adhabu hiyo inatokana na kukiuka kanuni mbalimbali za utangazaji na kanuni ndogo za wakati wa uchahuzi za mwaka 2015.

Kilaba amesema, Clouds TV na Redio walikiuka kanuni za utangazaji kwa kutangaza wagombea kupita bila kupingwa wakati wenye uwezo wa kutangaza ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Mnamo tarehe 26 Agosti 2020 kati ya saa 1 hadi 4 asubuhi kupitia vipindi Clouds 360 na Powerbreakfast Clouds Redio. Walirusha takwimu za wagombea ubunge waliopita bila kupingwa lakini wakijua taarifa hiyo haijathibitishwa na NEC na kukosa pia midhania,” amesema Kilaba.
 
Kutokana na ukiukwaji huo, Kilaba amesema, “kuanzia muda wa agizo hili saa 8 mchana leo mpaka mwisho wa siku hii ya leo, Clouds TV wanatakiwa kuahirisha matangazo yote na kutumia muda wote uliobaki kuomba radhi kwa Watanzania wote kwa kukiuka kanuni ya utangazaji kupitia kipindi chao cha Clouds 360.”

“TCRA imesitisha utoaji wa huduma za utangazaji kwa Clouds TV kuanzia kesho 28 Agosti 2020 hadi 3 Septemba 2020. Yaani hakuna kwenda hewani. Iwapo Clouds TV itashindwa au itakaa au itakaidi uamuzi huu, hatutakuwa na jinsi nyingine, tutachukua hatua zingine za kisheria na kiudhibiti,” amesema

Kilaba amesema, maagizo hayo kwa Clouds Tv yanafanyika pia kwa Clouds Redio kwa muda huo huo.


from MPEKUZI

Comments