Slaa:Anayeuza Asali Kwenye Vifungashio Vya Chupa Za Konyagi Na Bia Miezi 6 Jela/faini Milioni Moja Au Vyote Kwa Pamoja.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Afisa nyuki Mkuu wa         Wakala wa Misitu Tanzania[TFS]           Kanda ya kati ,Bw.Karengi             Slaa amebainisha kuwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2002 ya ufugaji wa nyuki ni marufuku kwa mtu yeyote kuuza asali kwenye vifungashio visivyo rasmi zikiwemo chupa za konyagi ,chupa za bia na chupa zozote za Mafuta zilizokwisha tumika bila kutoka moja kwa moja kiwandani.

Akizungumza na  mtandao huu Agosti 26,2020  Bw.Karegi alibainisha kuwa kuuzia asali kwenye chupa ambazo zilishatumika kuna weza sababisha madhara kwa mlaji hivyo ni vyema wajasiriamali wa asali wakazingatia usafi kwa kuhifadhi asali katika ndoo na chupa zilizotoka kiwandani moja kwa moja.

“Katika suala  la uuzaji wa asali katika chupa zilizotumika mfano katika chupa za konyagi,chupa za bia kwa kweli ni hatari kwa mlaji kwa hiyo nitoe rai tu kwa jamii kujitahidi  sana kuwa na desturi ya kununua vifungajishio moja kwa moja  kutoka kiwandani kwa sababu unapochanganya asali na chupa iliyokuwa na makaki ya bidhaa nyingine mfano,pombe na Mafuta panaweza kuleta madhara kwa mlaji ,na sheria ipo wazi ambapo kwa mujibu wa sharia ya mwaka 2002 ya ufugaji wa nyuki ni marufuku kwa mtu yeyote kuuza asali kwenye vifungashio visivyo rasmi zikiwemo chupa za konyagi ,chupa za bia na chupa zozote za Mafuta zilizokwisha tumika na na ikibainika fani yake ni Tsh.Milioni 1 au miezi sita jela au vyote kwa Pamoja”alisema.

Pia,afisa nyuki mkuu huyo amesema kuwa huwa wanafanya operesheni maalum kuhusu asali zinazochakachuliwa ikiwemo kuzidisha kiwango cha maji.

Aidha,Bw.Slaa amebainisha kuwa TFS kanda ya kati hadi sasa ina jumla ya Mashamaba ya asali 39 huku misimu ya urinaji wa zao  hilo muhimu hufanyika kwa misimu mikuu miwili ambayo ni Msimu mkuu unaoanzia mwezi April hadi Julai na Msimu mdogo unaoanzia Mwezi Disemba hadi Januari ya kila mwaka.

“Katika kanda yetu ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Morogoro,Dodoma na Singida kufikia hadi sasa tuna jumla ya mashamba 39 ya asali ambayo yanasimamiwa na TFS mashamba yote hayo yametundikwa mizinga na mzinga mmoja una uwezo wa kutoa wastani wa kilo 7 hadi 9  za asali na ikumbukwe kuwa kuna aina mbili za asali ambazo ni asali ya nyuki wakubwa na asali ya nyuki wadogo na asali ya aina yote ni bora kibiashara”alisema.

Hata hivyo,amesema kuhusu rangi ya asali huwa inategemea na aina ya mimea jinsi nyuki walivyokuwa wanatafuta maua ili waweze kutengeneza asali ambapo pia alibainisha kuwa asilimia 95% ya asali Tanzania inatokana na ufugaji asilia ambapo hutegemea uoto wa asili ,ushauri wa wataalam na wafugaji  wa jadi hutumia moshi katika suala zima la urinaji wa asali.

Kuhusu suala la Elimu Bw.Slaa kati ya Wilaya 17 zilizopo kanda ya kati,Jumla ya wilaya 10  zilifikiwa  kujengewa uwezo juu ya namna bora ya ufugaji wa nyuki ambapo ni saw ana takriban wajasiriamali 200 na  asasi za kiraia zisizopungua 5  zikijengewa uwezo huku mizinga 1000 ilisambazwa katika miaka mitatu iliyopita na mwitikio ukiwa mkubwa.

Baraka Christopher ni Mkurugenzi wa kampuni ya BEEKEEPING mkoani Dodoma  inayojishughulisha na utoaji elimu ya nyuki ,akizungumza na mtandao huu katika semina iliyokutanisha Wajasiriamali mbalimbali mkoani hapa Mwanzoni Mwa Juma hili  ukumbi wa ofisi za shirika la viwanda vidogovigogo [SIDO] alisema wao kwa kushirikiana na SIDO Pamoja na TFS wamefanikiwa kuwafikia wajasiriamali 40 mkoani hapa kutoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki huku akiwaasa watanzania kuchangamkia fursa ya ufugaji huo kwani una tija kubwa.

“Kwa kweli TFS,na SIDO wamekuwa mstari wa mbele kutupa support juu ya utoaji wa elimu ya ufugaji  wa nyuki na tumefikia wajasiriamali 40 kutoa elimu na nyuki wanatengeneza asali ngundi Pamoja na sumu hivyo elimu ya ufugaji bora wa nyuki panakuwa na urafiki wa mazingira”alisema.

Nao baadhi ya wanufaika wa Mafunzo hayo na wajasiriamali wa nyuki mkoani Dodoma   akiwemo Sifa Lubasi,Damas Kambagu na Veronica Peter walisema kuna umuhimu mkubwa kwa wajasiriamali kupata mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki na si kutegemea kuajiriwa huku wakibainisha kuwa kuna baadhi ya vijana mkoani hapa huwa ni wavivu wa kushiriki mafunzo lakini ni wepesi kuhudhuria masuala ya starehe hivyo ni muhimu vijana kubadilika.

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments