Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuongeza muda wa siku kumi za kuomba mkopo kuanzia kesho (Jumanne, Septemba 1, 2020) ili kuwawezesha wanafunzi waombaji mkopo ambao hawajakamilisha maombi yao ya kukamilisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amewaambia wanahabari jijini Dar es salaam leo (Jumatatu, Agosti 31, 2020) kuwa uamuzi huo unafuatia maoni, ushauri na maombi kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walezi ambao HESLB imepokea.
Maombi yaliyopokelewa hadi sasa
“Hadi leo asubuhi, tumeshapokea maombi 85,921 kwa njia ya mtandao, na kati ya hayo, maombi 71,888 sawa na asilimia 84 ni kamilifu na yana nyaraka muhimu na mengine 14,033 yanakosa nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi wa waombaji ambavyo havijathibitishwa na RITA au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar maarufu kama ZCSRA,” amesema Badru.
Badru ameongeza kuwa HESLB imeendesha programu za elimu ya uombaji mkopo kwa usahihi kwa wanafunzi katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kwenye kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako wamepokea maoni na maombi ya kuongezwa kwa muda na kutoa nafasi kwa wanafunzi waliopo kwenye kambi za JKT kuomba mkopo mara wamalizapo mafunzo.
“Kuhusu waliopo JKT hivi sasa, tunaendelea kuwasiliana na Makao makuu ya JKT ambao tunashirikiana kuhakikisha vijana wote wahitaji wanapata fursa bila kuathiri mafunzo ambayo ni muhimu,” amesema Badru.
Bajeti ya Mikopo kwa 2020/2021
Kuhusu bajeti ya fedha za mikopo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga TZS 464 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 145,000 wa taasisi za elimu ya juu na kati yao, 54,000 wanatarajiwa kuwa ni wa mwaka wa kwanza.
“Hili ni ongezeko la kutoka jumla ya TZS 450 bilioni zilizotolewa mwaka huu 2019/2020 ambazo zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,292 hadi sasa,” amesema Badru katika mkutano uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka RITA na Shirika la Posta Tanzania (TPC), taasisi zinazowahudumia waombaji mkopo.
Ushauri wa RITA na Posta
Akiongea katika mkutano huo, Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) Josephat Kimaro amewakumbusha wanafunzi waombaji mkopo waliowasilisha maombi ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi wao, kufungua barua pepe walizotumia kuwasilisha maombi yao RITA ili kupokea majibu.
Naye Meneja Mkuu anayesimamia Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mwanaisha Said amesema wamekubaliana na HESLB kuendelea kupokea nakala ngumu za maombi ya mikopo katika ofisi za TPC nchini kote na kuziwasilisha HESLB hadi Septemba 15 na kuwataka wanafunzi kutokuwa na wasiwasi na kutokupokelewa kwa bahasha zao.
Mwisho.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment