CCM Kuzindua Kampeni Zake Leo Kwa Kishindo

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema leo kinatarajia kuishangaza dunia wakati kikizindua kampeni za uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani katika Uwanja wa Jamhuri, jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alisema utakuwa uzinduzi wa aina yake ambao haujawahi kufanywa na chama chochote.

“Uwanja wa Jamhuri tutakuwa na jambo letu kesho (leo). Tutaisimamisha dunia. Halitakuwa jambo la kubahatisha, utakuwa uzinduzi babu kubwa,” alisema Polepole na kuongeza:

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipanga Agosti 26 kuwa ni siku ya kuanza kwa kampeni, lakini sisi tukajipa siku tatu za kuandaa mitambo yetu, sasa siku yenyewe imefika. Ratiba itaanza saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni.

“Kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana kutakuwa na ubunifu wa hali ya juu kutoka kwa wasanii wakieleza mafanikio ya Rais John Magufuli.”

Polepole alisema kuanzia saa 7:00 mchana shughuli rasmi za kampeni zitaanza na kwamba wanatarajia uwanja kufurika, hivyo kutafungwa Televisheni nje ya uwanja ili kuwawezesha Watanzania watakaoshindwa kuingia uwanjani kutazama.

“Matangazo yatakuwa mubashara kwa vyombo mbalimbali, mgombea wa CCM Rais John Magufuli ataelezea mafanikio katika miaka mitano, kuueleza ulimwengu mambo mazuri yaliyofanyika, changamoto tulizokutana nazo pamoja na mambo makubwa yaliyofanyika na yanayotarajia kufanyika,” alisema.

Aidha, Polepole alisema katika uzinduzi huo, wasanii mbalimbali wanatarajia kutumbuiza wakiwamo Diamond, Ali Kiba, Harmonize, Masanja, Hamza Kalala, Mrisho Mpoto, Lavalava, Beka Flavor, Shilole, G-Nako, Nandi, Maua Sama na Joti.




from MPEKUZI

Comments