TIC Yatahadharisha Wananchi Kuhusu Utapeli Wa Mitandao

Na Mwandishi wetu-Dar es Salaam.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimetoa tahadhari  kwa Umma kupuuza na kuepukana na utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wanaotumia jina na nembo ya Kituo  kutapeli watu, kwa kujifanya wanasimamia Uwekezaji nchini.

Taarifa ya TIC iliyosainiwa na Kaimu Afisa Habari na Uhusiano wa Taasisi hiyo Grace Semfuko imesema kuna Taasisi inayojiita “Tanzania Investments” ambayo inapatikana Jijini Mwanza imekuwa ikihamasisha watu kuchangia kwa ajili ya kupata huduma za uwekezaji na kwamba tayari imeundwa kundi la WhatsApp ambalo linahamasisha watu kujiunga na kupata huduma za uwekezaji nchini.

“Ieleweke wazi kuwa kundi hilo linafanya kazi zake kinyume cha sheria, na sisi tumeshatoa taarifa kwenye vyombo vya kisheria ili waweze kushughulikiwa, wanatumia nembo na majina ya kituo kuhalalisha utapeli wao, kituo cha uwekezaji tanzania ni Taasisi pekee inayofanya kazi za kuhamasisha uwekezaji tukisaidiana na taasisi nyingine kama EPZA na nyinginezo za Serikali zinazohusika na masuala haya” ilisema taarifa hiyo. 

“Kumezuka kundi la WhatsApp linalojiita TANZANIA INVESTMENTS ambalo linajinasibu kusimamia Uwekezaji nchini,kundi hili linajitambulisha kuwa linapatikana eneo la Nyanguge, Magu, Mwanza, Kundi hili  pia linatumia majina na nembo ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), pamoja na kuvunja sheria za nchikundi hili pia linafanya utapeli” ilisema taarifa hiyo.

Aidha,ilieleza kuwa katika kusogeza huduma za uwekezaji maeneo yote nchini, TIC imeanzisha Ofisi za Kanda saba (7) ili kuwafikia Wateja wake wote na kuwataka wadau kuzitumia ofisi hizo.

Ilizitaja kanda hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Kusini yenye Ofisi zake Mkoani Mtwara (Jengo la Mkuu wa Mkoa) inayohudumia Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye Ofisi zake  Mkoani Mbeya (Jengo la Benki ya NBC) inayohudumia Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe .

Kanda zingine ni pamoja na ya Kaskazini yenye Ofisi zake Mkoani Kilimanjaro(Ofisi za Mkuu wa Mkoa) inayohudumia Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Tanga, Kanda ya Mashariki yenye Ofisi zake Dar es Salaam (Jengo la TIC Makao Makuu) inayohudumia Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, Kanda ya Magharibi yenye Ofisi zake Mkoani Kigoma (Jengo la Mkuu wa Mkoa) na inahudumia Mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma na Tabora.

Aidha zipo pia Kanda ya Ziwa yenye Ofisi zake Mkoani Mwanza (Barabara ya Kenyatta), inayohudumia Mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga,Geita na Simiyu na Kanda ya Kati yenye Ofisi zake Dodoma (Jengo la Manispaa) inayohudumia Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.




from MPEKUZI

Comments