Takukuru Manyara Yawafunda Wasimamizi Wa Mizani Tanroads

Na John Walter-Babati
Watumishi kutoka Ofisi ya Wakala wa bara bara Mkoa wa Manyara (TANROADS) kitengo cha Mizani wametakiwa kufanya Kazi zao kwa uadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya kuharibu Kamera na mizani ili kuwezesha wasafirishaji kupita kwenye mizani kwa kukwepa tozo za mizigo iliyozidi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa dawati la Elimu kwa Umma kutoka Ofisi ya Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara Sultan Ng’aladzi wakati wa semina maalum kwa watumishi hao kuhusu Rushwa na athari zake.

Amewaambia watumishi hao kuwa vitendo hivyo hupelekea upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kwa rushwa kidogo wanayopokea ambayo hupelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara kutokana na kupitisha mizigo yenye uzito usiohitajika ambapo matengenezo yake huligharimu Taifa fedha nyingi ambazo zingeelekezwa katika matumizi mengine.

Semina hiyo iliwahusisha wadau wa usafiri na usafirishaji wakiwemo wamiliki wa magari ya mizigo na abiria pamoja na askari wa usalama barabarani.


from MPEKUZI

Comments