Mwongozo Wa Udhibiti Wa Maambukizi Ya Ugonjwa Wa Corona (Covid-19) Katika Shule, Vyuo Na Taasisi Za Elimu Nchini

Kufuatia Mlipuko wa Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) uliripotiwa kwa mara ya kwanza hapa nchini tarehe 16 Machi, 2020, Serikali ilichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu nchini. 


Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufunga shule zote za Awali, Msingi, Sekondari, Vyuo na taasisi za elimu nchini. Kutokana na takwimu za mwenendo wa ugonjwa huu nchini kwa sasa kuonyesha kupungua kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, mnamo tarehe 20 Mei 2020 Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ilitangaza uamuzi wa kurejesha ratiba za masomo kwa shule (Kidato cha 6), Vyuo na Taasisi za Elimu kuanzia tarehe 01 Juni 2020.  
 
Katika kuendeleza jitihada za kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Corona (COVID-19) nchini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa Mwongozo huu ambao unalenga kuweka mazingira wezeshi ya udhibiti wa maambukizi ya COVID-19 katika Taasisi za Elimu ikiwa ni pamoja na Vyuo, Shule za Sekondari na Shule za Msingi.  
 
Ili kufanikisha uwepo wa mazingira hayo, Mwongozo huu umezingatia maeneo makuu manne ambayo ni Maandalizi ya mazingira ya taasisi za elimu kabla ya kufunguliwa, Uchunguzi wa Afya, Usafiri wa kwenda na kurudi shuleni/Chuoni na Mazingira ya kujifunzia kama inavyoonekana hapo chini: - 

    i. Maandalizi ya Mazingira ya Taasisi za Elimu kabla ya kufunguliwa 
    a. Kutakasa (Decontamination) mazingira yote ya shule, Chuo au taasisi kwa kuzingatia miongozo ya utakasaji iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hii inahusisha taasisi ambazo zilitumika kwa ajili ya kutunza washukiwa au wagonjwa wa Corona. Utakasajii huu ufanyike angalau masaa 72 kabla ya wanafunzi kuingia.  
 
    b. Siku ya kwanza ya kufunguliwa shule, chuo au taasisi ya Elimu ni muhimu itumike kutoa elimu kwa wanafunzi/wanachuo na wafanyakazi wote kuhusu ugonjwa wa COVID-19 pamoja na dalili zake na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.  
 
    c. Kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono (sabuni na maji tiririka) kwa ajili ya usafi wa mikono katika kila eneo au maeneo ya madarasa, ofisi, kila geti/lango kuu, mabweni, maktaba, bwalo la chakula, vyoo na maeneo mengine muhimu. Wizara inasisitiza matumizi ya sabuni na maji tiririka ndiyo iwe njia kuu ya usafi wa mikono. Vilevile vifaa vya kunawa mikono vizingatie mahitaji ya wanafunzi/wanavyuo wenye ulemavu. Aidha, Vitakasa Mikono (Hand sanitizer) vinaweza kutumika kama mbadala wa maji tiririka na sabuni.  
 
    d. Uongozi wa Shule/Chuo uhakikishe vitakasa mikono (hand sanitizer) vinavyotumika vina ubora unaotakiwa (iliyotengenezwa kwa ethanol yenye asilimia zaidi ya 70) kwa wanafunzi na wanavyuo. Matumizi ya vitakasa mikono ni suala la hiari kwa mwanafunzi/mwanachuo kwa sababu Wizara tunasisitiza zaidi matumizi ya maji tiririka na sabuni.  
 
    e. Spirit (Methanol) isitumike kama kitakasa mikono katika maeneo yote ya shule, Chuo na taasisi. Wanafunzi wasiagizwe kwenda na spirit shuleni na Chuoni. Uongozi wa Shule/Chuo uhakikishe wanafunzi hawaingii na spirit katika maeneo/Taasisi zao.  
 
    f. Shule, Chuo au taasisi yenye vituo vya kutolea huduma za afya, watumishi wote wanaohusika wapewe elimu juu ya kuwahudumiwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote watakaoshukiwa kuwa na COVID-19 ikiwemo kuwapatia msaada wa kisaikolojia na kuondoa unyanyapaa. Aidha, Shule/Chuo/Taasisi hizi zinapaswa kuwa na dawa na vifaa kwa ajili ya dharura.  
 
    g. Uongozi wa Shule, Chuo na taasisi za Elimu zinazotoa huduma za kulaza wanafunzi (bweni) uhakikishe kadri inavyowezekana kunakuwepo na nafasi ya kutosha kati ya kitanda kimoja hadi kingine na kudhibiti uchangiaji vifaa kwa wanafunzi kama vile taulo, mashuka, vyombo vya kuogea na vifaa vya usafi wa mwili.  
 
    h. Uongozi wa Shule, Chuo na taasisi za elimu zihamasishe wanafunzi, walimu na wafanyakazi wao kuvaa barakoa za vitambaa (Cloth masks) wakati wanaporudi shuleni au vyuoni. Aidha, wazazi/walezi wahimizwe kuwapatia watoto wao barakoa za vitambaa kabla ya kwenda shuleni/Vyuoni.  
 
    i. Uongozi wa Shule, Chuo na Taasisi za elimu ziweke utaratibu mzuri wa upatikanaji wa barakoa za vitambaa  (Cloth Masks) zinazotengenezwa nchini na ambazo vinaweza kufuliwa na kupigwa pasi kila siku katika maeneo yao kwa gharama nafuu. Barakoa za vitambaa vya pamba zenye safu mbili (two layers) ndizo zinazoshauriwa kuvaliwa kwa kuwa ni bora na salama kiafya.Wazazi wanaweza kuwapa au kuwanunulia watoto wao.  
 
    j. Uongozi wa Shule, Chuo na Taasisi ya Elimu unapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuhifadhia taka zitokanazo na barakoa zilizotumika na kuziteketeza kama taka nyingine hatarishi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona. 

ii. Uchunguzi wa Afya;
 a. Wanafunzi watakaohisiwa kuwa na dalili za COVID-19 wafanyiwe vipimo kabla ya kurudi shuleni/chuoni. 
 b. Wanafunzi watakaobainika kuwa na maambukizi wabaki nyumbani hadi hapo hali zao za afya zitakapoimarika. 
 c. Kwa wanafunzi ambao watabainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona wakiwa Shuleni/chuoni, Uongozi wa Shule au chuo utoe taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu nao kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.


    iii. Usafiri wa kwenda na kurudi shuleni/chuoni: 
a. Wamiliki wa magari ya Shule/Chuo (School bus) waweke vitakasa mikono kwenye magari yao kwa ajili ya wanafunzi wakati wa kupanda kuelekea shuleni/Chuoni, 
b. Wamiliki wa magari ya Shule/Chuo (School bus) wahakikishe kuwa abiria na wahudumu wote wanavaa barakoa za vitambaa na kutumia vitakasa mikono kabla ya kupanda gari husika.
   
    iv. Mazingira ya kujifunzia:  
a. Uongozi wa Shule au Chuo unapaswa kuhimiza wanafunzi/wanachuo, walimu na watumishi wao kuzingatia Kanuni za Usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni kabla ya kuingia getini/lango kuu, darasani, bwenini, maktaba, bwalo la chakula, ofisini na maeneo mengine muhimu. Wizara inasisitiza matumizi ya sabuni na maji tiririka ndiyo iwe njia kuu ya usafi wa mikono. Aidha, Vitakasa Mikono (Hand sanitizer) vinaweza kutumika kama mbadala wa maji tiririka na sabuni. Inaelekezwa walimu wa madarasa wakisaidiana na viongozi wa wanafunzi/viranja wahakikishe haya yanasimamiwa ipasavyo.  
 
 b. Uongozi wa Shule au Chuo unapaswa kuhakikisha, kadri inavyowezekana, watumishi wote na wanafunzi/wanachuo wanakaa/kusimama kwa umbali utakaokuwa ni salama kati ya mtu mmoja na mwingine wawapo sehemu yoyote wakati wa mafunzo. 
 
    c. Uongozi wa Shule, Chuo na taasisi za elimu zihakikishe wanafunzi, walimu na wafanyakazi wao wanavaa barakoa za vitambaa (Cloth masks) wakati wote wawapo shuleni na vyuoni hususani wanapokuwa katika mikusanyiko ikiwa ni pamoja na darasani au katika vikundi vya majadiliano. Watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wanafunzi/walimu/watumishi wenye magonjwa ya moyo, selimundu (sickle cell) na wenye magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile pumu hawapaswi kuvaa barakoa.  
 
    d. Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu, walimu wanapaswa kuvaa barakoa maalum zitakazoruhusu mwanafunzi mwenye matatizo ya usikivu kuwasiliana na mwalimu.  
 
    e. Wataalam wa Afya wa Mkoa na Halmashauri husika washirikiane na Uongozi wa Shule au Chuo kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya barakoa, hatua sahihi za unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni na utumiaji sahihi wa vitakasa mikono kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Shule/Chuo husika.  
 
    f. Pale ambapo Shule, Chuo au Taasisi ina watumishi wenye taaluma ya afya, inashauriwa watumishi hawa watumike ipasavyo kutoa elimu ya COVID-19 na kusimamia Utekekelezaji wa Mwongozo huu kwa kushirikiana na Watalaam wa afya wa Mkoa na Halmashauri zao. 
 
    g. Ziara za mafunzo nje ya shule zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na maambukizi  ya COVID-19. 
 
    h. Uongozi wa Shule, Chuo au Taasisi ya Elimu zinahimizwa kuzingatia Matumizi ya TEHAMA katika kufundisha na kujifunzia ili kupunguza uwezekano wa maambukizi ya COVID-19. 
 
    i. Wataalamu wa Afya wa Mikoa na Halmashauri zote nchini wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika shule, vyuo na taasisi za elimu zilizoko katika maeneo yao ili kuhakikisha tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya COVID-19 zinazingatiwa kabla ya kufunguliwa Shule/Chuo na wakati wa masomo ikiwemo kutoa taarifa kwenye mamlaka husika. 
   
Mwongozo huu utaboreshwa mara kwa mara ili kukidhi mahitaji ya wakati husika. 


Ummy A. Mwalimu (Mb) 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, 
Jinsia, Wazee na Watoto 
27 Mei, 2020


from MPEKUZI

Comments