Jakaya Kikwete: Hostel za Magufuli Ziko Salama na tayari kwa matumizi, Vijana Njooni Muendelee na Masomo

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete amesema hosteli za chuo hicho maarufu hostel za Magufuli ambazo zilibadilishwa matumizi na kuwa karantini kwa watu waliokuwa wakitoka nchi za nje ikiwa ni hatua ya kupambana na corona, ziko salama na tayari kwa matumizi. 

Kikwete ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 28, alipotembelea hosteli hizo kwa ajili ya kukagua mazingira kabla ya wanafunzi kuanza kupokelewa kwa ajili ya kuendelea na masomo yao kuanzia Juni Mosi mwaka huu. 

"Tulitaka waliochukua ile hosteli watangaze rasmi kwamba wameshafanya yale yote waliyoahidi, ya kutayarisha hii hosteli kuwa salama kwa ajili ya kupokea wanafunzi wetu.  Kauli hiyo hatutakiwi kutoa sisi, wala DVC, tunataka watoe wenyewe waliochukuliwa hizo hosteli na waeleze walichokifanya kuhakikisha wanafunzi na jamii yetu kwamba hapa mahali pako salama, kwa hiyo Neema ( kwa niaba ya mganga mkuu wa mkoa Dar) nikushukuru kwa kauli uliyotoa, wamekusikia

"Niliposikia wanawaleta wasafiri kutoka nje na kukaa hapa kwa siku 14, shaka yangu kubwa ilikuwa, itakuwaje kama hao watu watakuwa na maradhi, je, wakiondoka hawataacha mbegu? Na vijana wetu wakija wakaja kupatia maradhi hapa?

"Lakini tukazungumza sana na uongozi wakanihakikisha kwamba serikali imechukua tahadhari zote kuhakikisha panakuwa  sterilized, disinfected kiasi cha kutosha ili wakija vijana pasiwe na shaka yoyote. Waliponieleza hivyo nilipata matumaini. Lakini nikawaeleza kuwa lazima tuhakikishe hilo limefanyika kwa sababu hatutaki hii kambi tukufu sana yenye jina la Rais… iwe ndio kitovu cha ugonjwa.

"Maana watu walikwenda makwao, isije ikatokea watakaporudi wakaugua wakasema si unaona serikali imewaleta na wametuachia mbegu za virusi. Hata tulipopata agizo la vyuo vifunguliwe mazungumzo yangu na DVC yslikues ni  kwamba tumejiandaaje. Akaniambia tumeshajiandaa vya kutosha ndipo siku ya pili yake ikatoka kwamba vyuo vifunguliwe Juni mosi

"Kwa maeleo yake ni kwamba hakuna hata mmoja miongoni mwa 426 waliogusana wale waliokutwa na maambukizi, 418 wametoka, kati ya hao hakuna hata mmoja aliyekutwa na virusi, kwa maana waliokuwepo hapa walikuwa salama ina maana kuwa hapa ni salama, ila makubaliano yetu ni lazima kufanya disinfection na wamefanya mwezi moja uliopita.

"Kwa hiyo tunaichukua kauli yenu kwamba pako salama, niwahakikishie vijana kwamba pako salama njooni, wale tuliowakabidhi wamefanya vile tulivyokubaliana, basi likitokea la kutokea tutawasiliana

"Lakini kwa upande wenu mmefanya tuliyoahidiana, kwa niaba ya uongozi wa chuo niwashukuru. Mmetimiza ahadi yenu, ndio uungwana. Ada ya mja hunena muungwana ni vitendo, mmenena lakini pia mmetenda." Amesema Kikwete


from MPEKUZI

Comments