Serikali itaendelea kuwalinda watumishi wa afya ili wasipate maambukizi wakati wakiwahudumia wagonjwa wenye Virusi vya Corona (COVID-19) kwa kuwapa vifaa kinga na mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa hao.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW) Ummy Mwalimu wakati wa kikao baina yake na wamiliki wa Hospitali binafsi na viongozi wa vyama vya kitaaluma vya afya.
Waziri Ummy alisema ni jukumu la Serikali kuhakikisha linawalinda watoa huduma za afya kwa kuwapa vifaa kinga ili wawahudumie wagonjwa waliopata maambukizi ya ugonjwa wa COVID -19.
“Ninaomba mzifikishe shukrani zangu za dhati kwa wahudumu wa afya ambao wako mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona ambao ni janga la kimataifa’’,alisema Waziri Ummy.
Waziri huyo pia aliwashukuru viongozi hao kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa kuhakikisha Hospitali zao zinatoa huduma kwa wagonjwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi alisema nguvu za pamoja zinahitajika ili wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa wa Corona na wale ambao hawajapata maambuzi waweze kupata huduma za matibabu kwa wakati.
Prof. Makubi alisema jambo la muhimu kwa watoa huduma za afya ni kujilinda wakati wanahudumia wagonjwa pia wamiliki wa Hospitali watoe elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya COVID -19 kwa wafanyakazi wao.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dkt. Elisha Osati aliipongeza Serikali kwa hatua iliyochukuwa ya kupambana na ugonjwa wa Corona nchini.
“Mkutano huu ni wa muhimu kwetu kwani tumekaa kwa pamoja na kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na ugonjwa wa COVID-19, ninaamini baada ya mkutano huu kila mmoja wetu ataenda kuyafanyia kazi”, alisema Dkt. Osati
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment