Safari Za Kwenda Kuwatembelea Ndugu Vijijini Zisubiri Corona iishe:- Dr Subi

Na WAMJW- DSM
Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi ametoa wito kwa wananchi kutosafiri kwenda vijijini kwa lengo la kuwasalimia ndugu katika kipindi hiki ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona kusambaa zaidi nchini.

Wito huo ameutoa leo, wakati akiongea na Waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam juu ya mwenendo wa kampeni ya “Mikono safi, Tanzania salama” inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

“Kwa wanaotaka kwenda kuwatembelea Wazee kijijini, wasubiri Corona iishe, kwasababu tunaona watu watatoka kwenye miji ambayo inamaambukizi wanaenda vijijini kuwatembelea wazazi ambao umri wao umeenda, inawezekana wana magonjwa ya uzeeni, kunauwezekano mkubwa wakuwaambukiza huko” alisema.

Aliendelea kusisitiza kuwa, katika maeneo yote yenye msongamano hususan maeneo ya biashara na huduma za Afya, waweke utaratibu mzuri, utaosaidia wateja kukaa umbali wa mita moja au zaidi pindi wanaposubiri kupata huduma, hali itayosaidia kukata mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

“Maeneo ya kutoa huduma mbali mbali, ikiwemo Hospitali na vituo vya Afya, waweke utaratibu mzuri, watu wanaokuja kupata huduma wakae katika utaratibu wa mita moja au zaidi ili watu hawa wasiweze kuambukizana maradhi, lengo likiwa kukata mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine ” alisema

Aliendelea kusema, ni muhimu uvaaji wa Barakoa uzingatiwe katika ngazi zote, hasa katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kuzichoma moto Barakoa zilizotumika ili kuepusha usambaaji wa magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.

“Tunasisitiza uvaaji wa Barakoa, hasa unapokuwa kwenye mkusanyiko wa watu, lakini barakoa sio kitu salama baada ya kumaliza kukitumia, kinakuwa kichafu na maambukizi, kwa mantiki hiyo, hakikisha unaitupa sehemu salama na unachoma moto ili mtu mwingine asiweze kuikokota na kuitumia tena ” alisema

Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, bado elimu ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka haijaeleleweka vizuri, hivyo kuitaka timu ya hamasa kuongeza nguvu katika hatua zote tano za unawaji mikono ili elimu hiyo isaidie katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

“Tunaposema kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni tunamaana kwamba, unapokwenda kunawa hakikisha sabuni imekolea vizuri kwenye kiganja cha mikono, hakikisha umesugua vizuri, povu la sabuni limeshika vizuri, na hakikisha umenawa vizuri mbele, nyuma, kwenye vidole na kila eneo la mikono vizuri kwa sekunde zisizopungua 20″alisema

Akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi wa kampeni ya “mikono safi, Tanzania salama,” Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ameweka wazi kuwa, mpaka sasa timu hiyo ya uhamasishaji imeshatembelea jumla ya maeneo 145 kati ya 213 yaliopangwa yametembelewa ikiwa ni sawa na asilimia 68.

Mbali na hayo amesema kuwa, licha ya kutoa elimu ya tahadhari, kikosi cha uhamasishaji kimekuwa kikitoa zawadi kwa taasisi na watu ambao wanazingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara, vikiwemo vitakasa mikono (Sanitizer), viang’azi (Reflectors) na khanga za Kampeni.


from MPEKUZI

Comments