Mgodi wa kuchimba dhahabu wa Geita (GGM) Kuanza Kutumia Umeme Wa Gridi Ya Taifa Mwezi Juni Mwaka Huu

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuanzia Mwezi Juni mwaka huu, Mgodi wa kuchimba dhahabu wa Geita (GGM) utaanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa kuendesha shughuli zake baada ya Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu mkoani Geita kukamilika mwishoni mwa Mwezi Mei, 2020.

Aidha alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho awali kilipangwa kukamilika mwezi Juni lakini kutokana na kasi ya ujenzi wake kitakamilika mwishoni mwa Mwezi Mei na kuanza kusambaza umeme kwa wateja ikiwemo GGM.

Dkt. Kalemani alisema hayo, alipofanya ziara ya kikazi Aprili 25, 2020, mkoani Geita ya kukagua ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu, Kituo cha kuchenjua dhahabu cha Geita na kuwasha umeme katika Kijiji cha Buyagu na Zahanati ya Musasa.

“Kituo hiki cha Mponvu kitakuwa mkombozi mkubwa wa nishati ya umeme ya kutosha na kwa gharama nafuu kwa wakzi wa Mkoa wa Geita na mikoa jirani,pia Mgodi wa GGM utajiendesha kwa faida zaidi na kuliongezea mapato taifa kwa sababu wataacha kutumia majenereta kuzalisha umeme ambao ni wa gharama kubwa sana ukilinganisha na umeme unaozalishwa hapa nchini” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa, mgodi wa GGM utatumia umeme wa gridi ya taifa kutoka kituo cha Mponvu ambacho kitapokea umeme wa njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 220 kutoka kituo cha Bulyanhulu mkoani Shinyanga hadi mkoani Geita yenye urefu wa kilomita 55.

Vilevile alieleza kuwa tayari njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 33 utakaotumiwa na mgodi huo yenye urefu wa Kilomita 6.5 kutoka katika kituo hicho hadi ndani ya mgodi huo imekamilika na kinachosubiriwa sasa ni kuunganisha umeme punde kituo hicho kitakapokamilika.

Dkt. Kalemani pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Buyagu,ambacho ni moja ya vijiji vinavyopitiwa na njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa njia hiyo kwa asilimia 80.

Katika kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini, aliwasha umeme katika zahanati ya Musasa na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulipia ili waunganishiwe umeme.

Hata hivyo aliliagiza Shirika la Umeme Nchini, ( TANESCO) kuharakisha ufungaji wa Mashineumba( Transfoma) katika kituo cha kuchenjua dhahabu mkoani Geita ambacho kiko katika hatua za mwisho kukamilika.

Dkt. Kalemani alirejea kusema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wote nchini wanaendesha shughuli za uchimbaji kwa kutumia nishati ya umeme unaozalishwa nchini kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema kuwa kituo hicho kikikamilika kitakuwa uwezo wa kuchenjua dhahabu inayotakiwa katika ubora wa kimataifa na kitawasaidia wachimbaji wadogo kunufaika zaidi na shughuli zao za uchimbaji tofauti na ilivyo sasa.

Gabriel aliwaomba wawekezaji kwenda kuwekeza zaidi katika mkoa huo wa Geita kwa kuwa kuna umeme mwingi wa kutosha na gharama nafuu kuendesha shughuli mbalimbali vikiwemo viwanda.

Vilevile aliishukuru Wizara ya Nishati kwa kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa na umeme wa kutosha ili kuvutia wawekezaji wengi, kuwaunganishia umeme wa bei nafuu wananchi wa mkoa huo pamoja na kujengwa kwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu ambacho kitawezesha migodi yote katika mkoa huo kutumia umeme, na kuugawa katika mikoa jirani. 


from MPEKUZI

Comments