Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ameipongeza Menejimenti ya Bodi ya Mkonge na watumishi kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuhamia katika ofisi iliyotwaliwa na serikali hivi karibuni kutoka kwa wamiliki binafsi.
Kusaya ametoa pongezi hizo jana (tarehe 27.O4.2020) Jijini Tanga wakati alipokwenda kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu mwezi Machi mwaka huu kufuatia ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu mali za bodi ya mkonge kumilikishwa kwa watu binasfi kinyume cha utaratibu.
“Nawapongeza menejimenti mpya ya Bodi ya Mkonge kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuhamia katika jengo hili na kuendelea na kazi za kusimamia zao la mkonge”alisema Kusaya
Waziri Mkuu aliagiza kuwa jengo lililokuwa linamilikiwa visivyo halali na Willian Kimweli Madundo na kulitumia kama Medicare hospital Tanga litumike kuwa makao makuu ya bodi kwani miaka ya nyuma ndipo palikuwa makao makuu ya Mamlaka ya Mkonge Tanzania .
Aidha,Katibu Mkuu huyo aliigiza bodi ya mkonge kuhakikisha inafuatilia mali zake ikiwemo nyumba 32 ambazo zilirejeshwa serikalini “ nataka waliokuwa wamiliki wapewe notisi na kuondoka au wapewe mikataba ya upangaji haraka” alisisitiza
“Bado kuna nyumba mbili nchini Uingereza,nataka zirejeshwe serikalini na zile nyumba mbili jirani na Mkonge hotel hapa Tanga zifuatiliwe kujua uhalali wa umiliki wake “ alisema Katibu Mkuu huyo
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Saad Kambona alimweleza Katibu Mkuu kuwa tayari wameanza kufanya kazi kwenye jengo jipya la ofisi kama walivyoagizwa na wamefanya ukarabati mdogo kuwezesha jengo hilo kutumika kama ofisi badala ya ofisi za zamani uwanja wa gofu Tanga .
Kambona alisema kwa sasa wanaiomba serikali kuendelea kuiwezesha bodi ili iweze kuhudumia zao la mkonge wakati ikijipanga kuanza kujitegemea kimapato.
‘Tuna lengo baada ya kuimarisha usimamizi wa zao la mkonge nchini,bodi iweze kutoa gawio kwa serikali “alisema Kambona.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa jitihada zake za kufufua zao la mkonge kwani ndio uti wa mgongo wawananchi wa Tanga.
Shigela alisema ni wakati sasa wizara ya kilimo ikaongeza msukumo katika kuhakikisha mbegu za mkonge zinapatikana kwa wingi na wakulima wanazipata kwa gharama nafuu. Mwisho
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
TANGA
28.04.2020
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment