Watano Watiwa Mbaroni Kwa Kumkata Mapanga Na Kisha Kumpora Afisa wa Serikali

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu watano wanaodaiwa kumkata mapanga kichwani ofisa wa serikali na kupora nyumbani kwake mali zenye thamani ya Sh. milioni 3.7.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma John (27), mkazi wa Bungu A, Japhet Charles (25) na Victor William (23), wote wakazi wa Chanika.

Kamanda Mambosasa aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Joseph Charles (28), mkazi wa Mbezi Juu na Anthony Christian (40), mkazi wa Temeke jijini.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa Machi 22 mwaka huu maeneo ya Tegeta wakiwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga na marungu.

“Watuhumiwa hawa walivamia nyumbani kwa Victor Nyirenda ambaye ni ofisa wa serikali na kumjeruhi kichwani kisha kupora simu mbili, kompyuta mpakato mbili aina ya HP, pochi na bahasha iliyokuwa na Sh. 500,000,” alisema.

Alibainisha kuwa watuhumiwa hao waliiba vitu vyenye thamani ya Sh. milioni 3.7 na baada ya taarifa kulifikia Jeshi la Polisi, ufuatiliaji ulianza na kuwakamata wote.

Kamanda Mambosasa alisema juzi walikamata watuhumiwa wengine wanne waliopokea vitu vya wizi kutoka kwa wahalifu wanaofanya matukio ya uvunjaji.

Alisema baada ya upekuzi kufanywa kwenye maduka ya watuhumiwa, walikamata kompyuta mpakato tatu, simu 10, luninga, deki na chaji za kompyuta.

Kamanda Mambosasa pia alisema jeshi hilo limekamata silaha mbili aina ya shotgun Pump Action na Maker Four.

Alisema silaha aina ya Shotgun Pump Action yenye namba za usajili 011822114, mali ya Kampuni ya Ulinzi ya OK Security, ilipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda Mambosasa alisema katika tukio hilo, wamewakamata walinzi wawili wa kampuni hiyo ambao ni Akili Mlatoni (31), mkazi wa Mtoni Mtongani na Isack Junia (22), mkazi wa Mwananyamala Ujiji.

Alisema silaha hiyo iliibwa Machi 19 mwaka huu katika Kanisa la EAGT City Centre Mtoni Mtongani.

Alisema silaha ya pili imekutwa imetelekezwa katika ghala la Kampuni ya Enka Enterprises na kwa sasa wanaendelea kumsaka mmiliki wake.


from MPEKUZI

Comments