Elimu juu ya Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona itolewe katika Maeneo ya Vijijini.

SALVATORY NTANDU
Wakazi wa mkoa wa Shinyanga wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wananchi wanaokaidi maagizo ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,Wazee na Watoto juu ya kujikinga na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya  Corona kwa kutonawa mikono kwa maji yaliyowekewa dawa za kuzuia maabukizi ya ugonjwa huo.

Hayo yalibainishwa Machi 28 na  Kisena Mihambo Mkazi wa Igwamanoni katika Halmashauri ya Ushetu mkoani humo baada ya kutembelewa na shirika lisilo la kiserikali la (REDCROSS) lililokuwa linatoa elimu kwa njia ya vipeperurishi na mabango kuhusina na kuchukua tahadhari juu ugonjwa unaosababishwa na virusi vya  Corona.

Alisema baadhi yao wamekuwa wakikaidi kutii maagizo ya serikali kwa kutonawa mikono hali ambayo inaweza kusababisha wakapatwa na maambukizi ya ugonjwa huo pindi utakapojitokesha na kuiomba serikali kupitia maafisa afya wa ngazi ya kata kuwachukulia hatua kali ili waweze kutii maagizo hayo.

“Katika Maeneo yote ya kutolea huduma za kijamii Serikali imeweka ndoo zenye Maji yaliyokwisha wekewa dawa za kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Corona lakini baadhi yetu tumekuwa wagumu kunawa mikono na badala yake tunaendelea kushikana mikono pindi tunaposalimiana”,alisema Mihambo.

Zubeda Ramadhani ni Mkazi wa Ntobo katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama alisema endapo wananchi wakihimizwa kwa kupewa elimu sahihi juu ya ugonjwa wa Corona na serikali hususani maeneo ya vijijini itawezakuzuia mlipuko wa virusi vya homa ya Mapafu (Corona).

“Tunaiomba serikali iwashirikishe viongozi wetu wa ngazi za mitaa,vijiji na kata ili kusaidia kuwafikia wakazi wengi hususani wakulima ambao kwa sasa wanaendelea na shughuli za uvunaji wa mazao mashambani ili kuwakinga na maambukizi ya Ugonjwa huo”alisema Ramadhani.

Kwa upande wake Mratibu wa RED CROSS Mkoa wa Shinyanga Samwel Katamba alisema Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la kuwahudumia  watoto Duniani (UNCEF) limewapa jukumu la kusambaza vipeperushi na Mabango nchi nzima kuhusiana na kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Corona.

“Tumeweza kuzifikia Halmashauri Sita  za mkoa wa Shinyanga kwa kuweka Mabango sambamba na kugawa vipeperushi vya ujumbe kuhusiana na ugonjwa huu wa Corona ikiwa ni pamoja na kutumia magari ya Matangazo lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu hii”alisema Katamba.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu Dk Nichodemas Senguo alisema mpaka sasa wameweza kutembelea kata 20 kwa kuwapatia elimu sahihi ya kujikinga na ugonjwa wa Corona huku mwitikio wa wananchi ukiwa ni mkubwa.

“Niwatake wananchi wa Ushetu waendelee kuzingatia maelekezo ya Wizara ya afya ya kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kutumia vitakasa mikono (Sanitaizer) sambamba na kuepuka kupeana mikono,pamoja na kujizuia kukaa kwenye mikusanyiko isiyokuwa na ulazima”alisema Dk Senguo.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments