Kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme wa jua ya ZOLA Electric Tanzania, ambayo zamani ilijulikana kama Mpower, imeeleza dhamira yake ya kusaidia jamii na kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha sekta ya elimu ambapo imetangaza kuwazawadia vifaa vya nishati ya umeme wa jua wanafunzi wa kidato cha nne watakaofanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa katika wilaya ya Kisarawe mwaka huu kupitia kampeni yake inayoendelea inayojulikana kama ‘Bukua na Ushinde’.
Akitangaza ofa hiyo ,Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ZOLA Tanzania, Yusuph Nassoro,amesema ‘Bukua na Ushinde’Imelenga kuchochea motisha kwa wanafunzi waliopo mashuleni kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani yao vizuri hususani katika maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme kutoka gridi ya taifa.
“Kampuni yetu tunaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na jamii ikielimika, inaweza kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka,ndio maana tumekuja na mpango huu wa kutoa motisha kwa wanafunzi mashuleni, hususani maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme ikiwa ni moja ya sera yetu ya kusaidia jamii sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini”,alisema Nassoro.
Alisema wanafunzi watakaofanikiwa kuingia katika 10 bora katika mithani ya taifa ya majaribio watapatiwa zawadi ya vifaa vya kusomea na wanafunzi watatu watakaofanikiwa kuingia katika 3 bora watafungiwa mitambo ya umeme wa sola kwenye familia zao sambamba na kupatiwa vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati hiyo kutoka kampuni ya ZOLA.
Nasoro,alisema mpango huo wa kusaidia wanafunzi utafanyika katika wilaya mbalimbali nchini ambako kampuni hiyo inaendesha shughuli zake, katika siku za karibuni ilitangaza ofa hiyo kwa wanafunzi wa sekondari katika wilaya ya Longido, mkoani Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameipongeza kampuni ya Zola, kwa kubuni mpango huu wenye lengo la kuinua sekta ya elimu kupitia kutoa motisha kwa wanafunzi “Nawapongeza Zola kwa kuja na ubunifu huu ambao utachangia kuinua sekta ya elimu katika maeneo ya vijijini vilevile kwa kuikumbuka wilaya ya Kisarawe”alisema.
Aliwataka wanafunzi kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili ziwasaidie kupata mafanikio na kukamilisha ndoto zao na watambue kuwa kusoma kwa bidii na kupata maarifa ni moja ya njia itakayowapeleka katika kupata mafanikio katika Maisha yao sambamba na kutoa mchango wa kuendeleza Taifa.
Alimalizia kutoa wito kwa makampuni mengine ya biashara kusaidia huduma za kijamii zenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko sambamba na kubuni biashara zinazochochea kuongeza fursa za ajira na kujiajiri kama ilivyo kampuni ya Zola.
Kampuni ya ZOLA Electric, ambayo zamani ilijulikana kama Mpower ilianza kutoa huduma zake nchini mwaka 2012 ikiwa inatoa huduma za neshati ya umeme wa jua na kuuza vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati hiyo
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment