Mwalimu ahukumiwa miaka 3 jela na kulipa fidia Mil.10 kwa kumsababishia ulemavu mwanafunzi wake

Na Amiri kilagalila,Njombe
Mahakama ya wilaya ya Njombe imemhukumu mwalimu Focus Mbilinyi aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Madeke hapo awali kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya shilingi milioni kumi baada ya kumkuta na hatia ya kumpiga mwanafunzi wake na kumsababishia ulemavu wa kudumu.

Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya wilaya ya Njombe kupitia hakimu Ivran Msaki ambae amesema mahakama imesikiliza ushahidi wa pande zote mbili wa shauri namba 141 la mwaka 2019 na kujiridhisha pasina shaka kuwa mtuhumiwa Mwal. Focus Mbilinyi alitenda kosa hilo.

Hakimu Ivran Msaki amesema kwamba kupitia mashahidi watano upande wa mtoa mashtaka na kwa kuzingatia ushahidi wa madaktari wa hospital ya mhimbili kitengo cha mifupa MOI uliowasilishwa na daktari Silvery Mwesigye mahakamanai hapo mahakama imemtia hatiani mwalimu Focus Mbilinyi Kwa kuhusika na kosa hilo.

Mahakama imeeleza kuwa mwalimu Focus Mbilinyi alimuadhibu mwanafunzi Hosea Manga kwa  mtindo wa kumningi’iniza miguu ikiwa juu ya dirisha huku kichwa kikiwa chini hali iliyompelekea kuanguka na kuvunjika kwa visahani vya uti wa mgongo na kumsababishia ulemavu.

Shauri hilo limesimamiwa na mawakili watatu upande wa utetezi ambao ni Innocent Kibadu , Lilian Gama na Octavian Mbugwani huku upande wa serikali ukiwakilishwa  Wakili msomi na Elizabeth Malya na jumla ya mashahidi 8 wa pande zote mbili.

Kupitia kifungu cha sheria namba 235 kifungu kidogo cha cha 1 cha kanuni ya adhabu namba 20 mahakama imemtia hatiani mwalimu focus mbilinyi na kumhukumu kifungo cha miaka  mitatu jela na Kupitia kifungu cha sheria namba 348 kifungu kidogo cha cha kwanza cha kanuni ya adhabu namba 20 mahakama imemtaka mwalimu huyo kulipa fidia ya fedha kiasi cha Shilingi Milioni kumi kwa kumsababishia ulemavu mtoto Hosea Manga.

Ikumbukwe kwamba mwalimu Focus Mbilinyi anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo tarehe 21 mwezi March mwaka 2017 huko kijiji cha Madeke kilichopo wilaya na mkoa wa Njombe.

Hata hivyo mahakama imetoa nafasi ya siku thelathini kukata rufaa endapo upande wa utetezi haujaridhika na adhabu iliyotolewa.


from MPEKUZI

Comments