Mahakama yaruhusu Rugemarila kuleta hoja za kutaka aachiwe huru

Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu imekubali kupokea hoja za maombi ya mfanyabiashara James Rugemalira anayetaka kuondolewa kwenye kesi ya utakatishaji fedha wa Sh. Bil 309.4.

Hatua hiyo inakuja wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa utetezi, John Chuma amedai kuwa mteja wake ameshawasilisha hoja za pingamizi la awali lakini hajapata majibu yoyote kutoka upande wa Jamuhuri.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai baadhi ya nyaraka amezipata leo mahakamani hapo na kuwa upande wa Jamhuri upo tayari kusikiliza hoja hizo kwa njia ya mdomo kama nyaraka hizo zimeshaingizwa kwenye kumbukumbu ya mahakama hata kwa wakati huo kama ratiba ingeruhusu.

Wankyo amedai mshtakiwa wa pili amekua anajiwasilisha mwenyewe huku akiwa na uwakilishi wa mawakili hivyo anapaswa kusema kama amewaacha ama wanaendelea.

Akijibu suala hilo, Rugemarila amedai kuwa amekua na wawakilishi hata zaidi ya thelasini lakini kuna hoja lazima aziwasilishe mwenyewe na kuwa hilo jambo walitakiwa kulalamika mawakili wake na sio yeye kwani sheria inamruhusu kujiwakilisha.

Baada ya hoja hizo, Hakimu Shaidi Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2020 litakapokuja kwa ajili ya  kutajwa na upande wa jamuhuri kuwasilisha majibu.

Mbali na Rugemalira, washitakiwa wengine ni Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power (IPTL) na Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.


from MPEKUZI

Comments