JWTZ Yakamata Silaha za Kivita Makambi ya Wakimbizi Katavi

Serikali ya  Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Jeshi la  Wananchi kikosi cha 202 na 401  wamefanikiwa  kukamata Bunduki 50 zikiwemo 13 za kivita na tatu zilizotengenezewa nchi za ulaya aina ya  G3 kufutia masako uliofanywa kwa muda wa siku 21 katika Makazi ya wakimbizi ya Katumba na Mishamo humo

Operesheni hiyo imefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mwezi Oktoba  mwaka jana wakati wa ziara yake  Mkoani Katavi kwa uongozi wa Serikali ambapo aliwataka   kuhakikisha wanawakamata watu wote ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria na wanaoingiza Silaha kutoka Nchi ya Burundi kwa ajili ya kufanyia  ujambazi na uwindaji haramu wa wanyama pori

 Akitoa taarifa ya operesheni hiyo inayojulikana kwa jina la Operesheni safisha Katumba  2020 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera ,Mkuu wa  Briged ya Magharibi  Brigedia  Jenerali  Jacob Mkunda  alisema kuwa  katika   operesheni hiyo walikamata bunduki 50.

 Alifafanua kuwa katika bunduki hizo walizofanikiwa kuzikamata ni bunduki za kivita 13 aina ya SMG , Bunduki tatu aina ya G3, Raifo moja  na Gobole  33.

Aidha wamekamata risasi 28 na mitego ya kukamatia wanyama 13

 Brigedia  Generali  Mkunda  alieleza kuwa katika msako huo wameweza kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa  17 ambao ni Raia wapya wa Tanzania wenye asili ya nchi ya Burundi  katika ya watuhumiwa hao  wanne wamekamatwa katika Makazi ya Wakimbizi ya Katumba Wilaya ya Mpanda na  14 wamekamatwa  katika Makazi ya Wakimbizi ya Mishamo Wilaya ya Tanganyika

Alisema kuwa kwenye msako huu wameweza kubaini uwepo wa  viwanda  vya kutengeneza  bunduki aina ya gobole kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo ambazo zimekuwa  zikitumika katika kufanyia  ujangili wa kuua wanyama kwenye Hifadhi  ya Taifa ya Katavi na kwenye mapori ya akiba .

 Nae  Mkuu wa oparesheni  hiyo safisha Mishamo na Katumba  Kanali  Evance  Mallaso  alieleza kuwa  wakazi wengi wanaoishi kwenye makazi hayo ya Katumba na Mishamo  wamekuwa na tabia  ya kuishi kwa usiri mkubwa wa kutowataja wahalifu wanaoingiza silaha kutoka nchi ya Burundi .

 Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera  alisema kuwa vyombo vya usalama katika Mkoa wa Katavi vimefanya kazi kubwa  katika kufanikisha  kukamatwa  kwa silaha hizo

 Amewaonya watanzania ambao  wanaoishi kwenye makazi hayo ambao wamekuwa  wakiwapokea wageni  wanaoingiza silaha  kutoka nchi za jirani  kwa kuzificha kwenye ndoo na kwenye madumu wanapozisafirisha wanaofanya hivyo watambue kuwa  na wao wakibainika watakamatwa tuu kwani Mkoa huu vyombo vya usalama  vipo kazini muda wote .

 Homera alieleza kuwa zoezi hilo la kuwasaka wanaomiliki silaha kinyume  na sheria ni endelevu linaendelea hivyo hakuna mwalifu yoyote ambae ataweza kushindana na vyombo vya dola .

 Alisema wakati wa ziara ya Rais Magufuli aliyoifanya oktoba 10 mwaka jana  alisikitishwa sana na tabia ya  waliokuwa   raia wa nchi ya Burundi waliopewa uraia wa Nchi ya Tanzania  wanaoishi kwenye Makazi  hayo kujihusisha na uingizaji wa silaha za kivita, ujambazi na ujagili hali ambayo ilimfanya Rais atowe agizo la kufanyika msako wa mara kwa mara


from MPEKUZI

Comments