Ethiopia Yatangaza Kutoshiriki Mazungumzo Marekani Kuhusu Ujenzi wa Bwawa Linalochota Maji Mto Nile Ambalo Misri Inalinga Vikali

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, haitashiriki mazungumzo ya pande tatu yaliyopangwa kufanyika leo Alhamisi mjini Washington, kwa lengo la kukamilisha makubaliano kuhusu matumizi ya bwawa la An-Nahdhah linalojengwa na nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maji, Umwagiliaji na Nishati ya Ethiopia imeeleza kuwa, nchi hiyo haitashiriki mkutano wa leo wa Washington kwa sababu mashauriano na wadau wa ndani ya nchi hiyo bado hayajakamilika.

Mazungumzo ya pande tatu ya mjini Washington kati ya Ethiopia, Misri na Sudan yanayodhaminiwa na serikali ya Marekani yanalenga kuupatia suluhu mzozo wa bwawa kubwa la maji la Al-Nahdhah linaloendelea kujengwa na serikali ya Ethiopia katika delta ya mto wa Blue Nile.

Katika mazungumzo hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo, wawakilishi wa Misri, Ethiopia na Sudan walitazamiwa kukutana kwa lengo la kukamilisha makubaliano rasmi kabla ya kuyasaini ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Ujenzi wa bwawa la An-Nahdhah ulianza rasmi mwaka 2011 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2020 kabla ya kuanza kutoa maji mwaka 2022.

Misri inapinga mradi wa ujenzi wa bwawa wa Al-Nahdhah kwa hofu kwamba utazuia mmiminiko wa maji ya Mto Nile inayoyategemea kwa takribani asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji.

Soma Pia:   Nafasi Mpya za Kazi Serikalini...Mwisho Mwezi wa Tatu

Hata hivyo serikali ya Addis Ababa inasisitiza kuwa mradi huo una ulazima kwa maendeleo ya taifa ili kuwatoa kwenye umasikini mamilioni ya raia wake.


from MPEKUZI

Comments