Asilimia 95 Misenyi ni Wahamiaji Haramu,Serikali ya Tanzania yatoa tamko

Na Mwandishi Wetu,Misenyi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni ameitaka idara ya uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),kuongeza nguvu kazi katika Wilaya ya Misenyi baada kugundulika uwepo wa wahamiaji haramu wengi wanaotishia hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Kagera unaopakana na nchi za Uganda na Rwanda.

 Ameyasema hayo baada ya kusikiliza taarifa ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya  Misenyi iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Kanali Denis Mwila iliyoweka wazi  idadi ya asilimia 95 ya wakazi katika Kata ya Kakunyu iliyopo Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ni wahamiaji haramu huku sababu kubwa zikitajwa za ongezeko hilo ni  kuletwa kwa wahamiaji hao kutafuta ajira na kutafuta mashamba ya maeneo ya malisho ndani ya Ranchi ya Taifa.

“kuna haja ya kuleta nguvu kazi  kubwa sana kutoka idara ya uhamiaji na NIDA,lazima tuwe na takwimu halisi ya kila mtu aliyeko katika maeneo haya ambayo yana mashaka,nchi yetu inakaribia kufanya uchaguzi mkuu ndani ya mwaka huu,tunahitaji kuwa salama ili kuweza kufanya uchaguzi pasina shaka yoyote ya uvunjifu wa amani ,tatizo hili ni kubwa linahitaji utatuzi wa haraka ili kuepuka madhara huko mbeleni” alisema Masauni

Akitoa taarifa ya idara ya uhamiaji kwa kipindi cha Januari hadi Disemba, 2019, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Denis Mwila, alisema idara ilitoa hati ya dharura za kusafiria 1,276 zenye thamani ya Shilingi 25,520,000/- huku makusanyo hayo yakikisiwa kuwa ni wastani wa makusanyo 2,126,666/- kwa mwezi huku idara ikikamata wahamiaji haramu 206 kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Disemba,mwaka jana.

“Tumekua na matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika wilaya yetu mfano katika kata ya Kakunyu watu 6,630 walisajiliwa huku raia halali wakiwa 319 tu,hivyo takribani asilimia 95 ya wakazi hao sio raia au uraia wao una mashaka,wahamiaji hao ni gharama kuwahudumia maana bado wana haki ya kuhifadhiwa na kupata mahitaji yote ya kibinadamu” alisema Kanali Mwila

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wahamiaji hao waliomba kupatiwa nauli ili warejee katika nchi zao huku wengine wakitaja  sababu ya kuingia nchini kinyume na sharia ni kuja kutafuta ajira na kukimbiwa na wenza wao.


from MPEKUZI

Comments